Umoja wa Mataifa wakabiliwa na ukata

Wednesday October 9 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema taasisi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya fedha.

Geterres alisema hali hiyo imetokana na wanachama wake kutolipa michango kwa karibu muongo mmoja sasa.

Katibu huyo alisema hayo leo Jumatano Oktoba 9 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekeni.

“Nchi wanachama 64 kati ya 193 hazijalipa michango yao ya kila mwaka mpaka sasa,” alisisitiza katibu huyo,

Guterres ameitaja Marekani ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa kuwa imeshindwa kulipa michango yake kwa muda mrefu.

Alisema endapo fedha hizo hazitatolewa, Umoja huo utashindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake na wanaotoa huduma.

Advertisement

Awali msemaji wa Umoja huo, Stephane Dujarric alisema kuwa tayari katibu mkuu huyo ameziandikia barua nchi zote wanachama akisema umoja huo uko katika hatari ya kuimaliza akiba yake ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema mpaka sasa nchi 129 zimelipa Dola bilioni 1.9 kama ada zao kwa mwaka 2019 pekee.

“Mwanachama aliyelipa pesa zote hivi karibuni ni Syria ambayo ndiyo inafikisha idadi ya nchi 129. Hadi sasa nchi wanachama wamelipa Dola bilioni 1.99 kuelekea katika tathimini ya bajeti ya kawaida ya mwaka 2019.”

Alisema Kiasi ambacho bado hakijalipwa mwaka huu ni Dola bilioni 1.3.

Dujarric alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba, nchi wanachama zilikuwa zimelipa asilimia 70 ya fedha jumla ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 78 katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.

Advertisement