Urusi yalaumu wapinzani Bolivia kusababisha Morales ajiuzulu

Urusi na Mexico zimeushutumu upinzani nchini Bolivia kwa kuanzisha machafuko katika nchi hiyo ya Amerika Kusini na kusababisha Rais Evo Morales ajiuzulu.

Urusi imesema matumaini ya serikali ya kufanya mdahalo yalipigwa kikumbo na mapinduzi yaliyopangwa, huku Mexico kupitia wizara yake ya Mambo ya Nje imelishutumu jeshi kwa kuingilia kati kinyume na Katiba.

Juzi Rais Morales alitangaza kujiuzulu akisema anachukua hatua hiyo kutuliza machafuko yaliyoikumba nchi hiyo tangu ulipofanyika uchaguzi uliozusha utata, wapinzani wakisema ulikumbwa a dosari nyingi.

Hatua ya Morales pia imezusha hofu ya kuzuka machafuko zaidi baada ya kusema amepinduliwa na anakabiliwa na hatua ya kukamatwa.

Wizara ya Mambo ya Mje ya Urusi imesema hali iliyojitokeza Bolivia imesababishwa na upinzani na hawakumpa nafasi Morales kukamilisha muda wake madarakani.

Urusi imetoa mwito wa utulivu katika nchi hiyo ikisema inatarajia kwamba nchi zenye nguvu hazitaingilia mambo ya ndani ya Bolivia.

Morales hajawasiliana na Urusi na wala hajaomba hifadhi katika nchi hiyo lakini jana Mexico ilisema iko tayari kumpokea na kumpa hifadhi ya kisiasa.