Uturuki yaanza kuwarejesha kwao wapiganaji wa IS

Muktasari:

 Wapiganaji wa kundi la wapiganaji la Islamic state (IS) wanaoshikiliwa na Uturuki wameanza kurudishwa kwenye mataifa yao. Wapiganaji hao wanatoka katika nchi za Ujerumani, Denmark, Marekani, Ireland na Ufaransa.

Ankara. Serikali ya Uturuki imeanza kuwarejesha kwenye mataifa yao wapiganaji wa kigeni wa kundi la Islamic state wanaoshikiliwa kama wafungwa katika Taifa hilo.

Wafungwa hao wanatoka katika nchi za Ujerumani, Denmark na Marekani na katika mpango wa kuwarejesha makwao, Uturuki imelaumu mataifa ya Ulaya kwa kuchelewa kuwachukua raia wake waliokwenda kupigana Syria.

Uturuki imesema imewakamata wanamgambo 287 katika eneo la Kaskazini mwa Syria na tayari inawazuia mamia ya washukiwa wa kundi hilo la kigaidi lililotekeleza mashambulizi kadhaa

Kwa mujibu wa ripoti ya DW, wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Suleyman Soylu amesema kuwa nchi yake ingeanza kuwarejesha katika mataifa yao wapiganaji wa kigeni wa IS kuanzia Jumatatu hata kama mataifa yao yamewafutia uraia wao.

Msemaji wa wizara hiyo, Ismail Catakii alinukuliwa akisema tayari raia  wa Marekani na Ujerumani walisharejeshwa makwao. Hata hivyo, hakutaja walikopelekwa licha ya Uturuki kusema wafungwa hao watarejeshwa katika mataifa yao asilia.

Watu wengine 23 watakaorejeshwa nchini kwao katika siku chache zijazo wote ni kutoka mataifa ya Ulaya ikiwa ni pamoja na raia mmoja wa Denmark, wawili wa Ireland, tisa wa Ujerumani na 11 kutoka Ufaransa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema Uturuki imeifahamisha kuhusu watu wake 10, wakiwemo wanaume watatu, wanawake watano na watoto wawili.

Msemaji wa wizara hiyo amesema kuwa hafahamu iwapo watu hao ni wapiganaji wa kundi hilo la wanamgambo la IS, lakini wizara haikupinga kuhusu uraia wao.

Wizara hiyo imesema watu saba wanatarajiwa kuwasili Alhamisi ijayo na wawili siku ya Ijumaa. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Horst Seehofer, amewahakikishia raia wa Ujerumani kuwa kila kisa kitachunguzwa kikamilifu na maofisa wa serikali ya Ujerumani na kwamba watafanya kila wawezalo kuwazuia watu hao watakaorejeshwa kwa kuwa na ushirikiano na kundi la IS wasiwe tishio nchini Ujerumani.

Wakati Serikali za Ujerumani na Denmark zikithibitisha kuwa zinafahamu kuhusu mipango ya Uturuki, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly, amesema hakufahamu kuhusu hatua hiyo.

Marekani haikujibu mara moja kuhusu tangazo hilo Uturuki. Gazeti la Sabah nchini Uturuki lililo na ukaribu na serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan limeripoti kuwa raia wa Marekani aliyerejeshwa nchini kwao  amekwama katika eneo lisilo na umiliki lililo na ulinzi mkali wa kijeshi kati ya mipaka ya Ugiriki na Uturuki.