VIDEO: Afanyiwa upasuaji kichwani huku akipiga ala ya muziki

Muktasari:

Mwanamuziki huyo aliamshwa katikati ya operesheni na kupewa kifaa chake cha muziki ili akicheze kuwezesha mkono wa kushoto kusogeasogea na hivyo upasuaji kufanikiwa.

London, Uingereza . Mpiga violin amewasaidia madaktari wa upasuaji kuepuka kuharibu ubongo wake wakati wa wakimfanyia operesheni ya kuondoa uvimbe kichwani kwa kucheza kifaa hicho cha muziki, hospitali ya Uingereza ambayo ilimfanyia upasuaji huo wa kibunifu, imeeleza.
Madaktari hao walipata mbinu hiyo mpya kuhakikisha maeneo tatanishi ya ubongo wa Dagmar Turner ambayo mikono inapita, hayaathiriwi wakati wa mchakato huo wa kuondoa uvimbe.
Turner, mwanamuziki mwenye umri wa miaka 53 akiwa na kundi la Isle of Wight Symphony Orchestra la kusini mwa England, aligundulika kuwa na uvimbe uliokuwa unakua taratibu mwaka 2013 baada ya kupoteza fahamu wakati akitumbuiza katika tamasha.
Baadaye akaamua afanyiwe upasuaji.
Profesa Keyoumars Ashkan, mshauri wa masuala ya nyurolojia katika hospitali ya King's College kusini mwa London, aliamua kutumia mpango huo kwa ajili ya kulinda seli zilizo sehemu ya kulia ya mbele ya ubongo wake.
Eneo hilo liko karibu na sehemu ya ubongo ambayo inadhibiti kutembea kwa kiasi kidogo cha mkono wa kushoto ambacho kilihitajika kuratibu pigo jepesi la violin.
Timu ya madaktari ilipendekeza kwamba Turner aamshwe katikati ya operesheni ili aweze kupiga violin yake na wakati huo aangaliwe kuhakikisha uhusiano hauathiriwi.
Picha za video zinamuonyesha Turner akicheza violin huku madaktari wakifuatilia katika compyuta.
"Huwa tunaondoa uvimbe kwa watu 400 kwa mwaka, kazi ambayo huhusisha kuwataka wagonjwa kufanya jaribio la lugha, lakini upasuaji huu ni wa kwanza kwa mgonjwa kucheza kifaa cha muziki," alisema Ashkan katika taarifa ya hospitali iliyotoka juzi.
"Tulifanikiwa kuondoa asilimia 90 ya uvimbe, yakiwemo maeneo yote yanayohisiwa kuwa hali mbaya, huku tukihakikisha mkono wa kushoto unaendelea kufanya kazi kikamilifu," alisema.