Virusi vya corona vyaingia Burundi

Muktasari:

Nchi hiyo ilikuwa ni miongoni mwa mataifa sita barani Afrika ambayo yalikuwa hajajaambukizwa na virusi vya corna.

Bujumbura, Burundi. Serikali ya Burundi imethibitisha ugonjwa wa corona (covid-19), umeingia nchini humo.

Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Thadee Ndikumana alisema jana kuwa raia wawili wa Burundi wamethibitika kuwa na maambukizi ya corona.

Waziri Thadee alisema wagonjwa hao wanaume, mmoja ana umri wa miaka 56 na mwingine 42 waliwasili kutoka Rwanda na Dubai.

Awali msemaji wa ofisi ya Rais, Jean Claude Karerwa alikaririwa na Shirika habari la BBC kuwa Mungu atawalinda na maambukizi haya kwasababu ameiweka Serikali ya Burundi katika sehemu ya kipekee.

Karerwa alisema endapo hali ya maambukizi itazidi Serikali itahairisha Uchaguzi Mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Wiki iliyopita Serikali ya Burundi ilitangaza kuchukua hatua za kuziua maambukizi ya corona pamoja na kusitisha ndege zote kwa muda wa siku saba.