Wafuasi Morales washinikiza arejee nchini kugombea tena wa urais

Muktasari:

Kiongozi huyo wa zamani wa Bolivia kwa sasa yuko uamishoni nchini Mexico. Hata hivyo, Rais wa mpito amesema kuwa Morales amepoteza sifa za kugombea tena urais

LA PAZ, Bolivia, Rais wa mpito wa Bolivia, Jeanine Anez amefuta uwezekano wa kiongozi aliyeko uhamishoni, Evo Morales kugombea katika uchaguzi mpya ujao.

Rais Anez alisema hayo jana Alhamisi Novemba 14 wakati maelfu ya waandamanaji wakimiminika katika barabara za mji mkuu La Paz kumuunga mkono kiongozi huyo aliyejiuzulu.

Waandamanaji hao walimtaka kiongozi huyo arejee nyumbani wakidai kwamba kung'atuka kwa Morales ni matokeo ya mapinduzi.

Mapema jana asubuhi mara baada ya kiongozi huyo wa mpito kuapishwa alitangaza mazungumzo na chama cha Morales cha Movement for Socialism (MAS) yameanza katika jaribio la kuleta amani katika nchi hiyo.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 52 alisema Morales hawezi kushiriki katika uchaguzi mwingine wowote mpya kwa sababu Katiba ya Bolivia inamzuia Rais kuongoza kwa mihula miwili mfululizo.

Alisema kutokana na hali hiyo chama chake cha MAS kinahitajika kumtafuta mgombea mwingine ili kushiriki uchaguzi huo.