Waingereza waanza kupiga kura

Muktasari:

Wananchi wa Uingereza wameingia katika uchaguzi leo ambako jumla ya wabunge 650 watachaguliwa.

London, Uingereza. Wananchi wa Uingereza wameanza kupiga kura kuchagua wabunge wao.

Chaguzi huu ambao ni wa kwanza kufanyika mwezi Desemba katika historia ya nchi hiyo utahusisha nafasi za wabunge 650 ambako utashirikisha zaidi ya watu milioni saba.

Hii ni mara ya tatu kwa Uingereza kupiga kura ndani ya miaka mitano. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 2015 na kufuatia wa 2017. Kwa kawaida uchaguzi nchini humo hufanyika kila baada ya miaka minne au mitano.

Vituo vya kupiga kura ndani ya maeneo 650 kutoka Wales, Uskochi na Kaskazini mwa Ireland vimefunguliwa leo kuanzia saa 1.00 asubuhi.

Shirika la habari la Ufaransa (AFP), liliandika kuwa kura zitaanza kuhesabiwa kuanzia saa 4.00 usiku mara baada ya vituo kufungwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo, matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa kuanzia Ijumaa asubuhi.

Jumla ya wabunge 650 watachaguliwa kwa kutumia mfumo wa 'first-past-the-post' ambao unatumika katika uchaguzi mkuu.

Katika mfumo huo wapiga kura huchagua yule wanayemtaka na mgombea atakayepata kura nyingi zaidi ndiye atakaeibuka mshindi.

Mwaka 2017, Newcastle ya kati ilikuwa ya kwanza kumaliza kuhesabu kura na kutangaza matokeo saa moja baada ya vituo kufungwa.

Uchaguzi huo unakuja miezi miwili baada ya wabunge nchini humo kupiga kura kutaka uchaguzi wa pili ufanyike.

Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika katika msimu wa baridi tangu mwaka 1974 na wa kwanza kufanyika mwezi Disemba tangu mwaka 1923.

Maelezo kuhusu sehemu za kupiga kura yanaweza kupatikana katika tovuti ya tume ya uchaguzi na pia yameorodheshwa katika kadi zinazotumwa kwenya nyumba za watu.