Walioambukizwa corona Rwanda wafika 70

Muktasari:

Serikali ya Rwanda imeaanza kugawa chakula bure kwa wananchi wake baada ya kutangaza amri ya watu kusalia nyumbani

Kigali, Rwanda. Watu wengine 10 wamethibitika kuambukizwa virusi vya corona (covid-19) nchini Rwanda.

Idadi hiyo mpya inafanya walioambukizwa virusi hivyo sasa kufikia 70.

Katika hotuba yake kwa taifa Rais Paul Kagame alisema idadi hiyo itaendelea kuongezeka kwa sababu wale waliotangamana na waathirika wanaendelea kutafutwa.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Rwanda, wagonjwa hao waliingia nchini humo wakitokea katika nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu sita walitoka Dubai, wawili Afrika Kusini na mmoja Afrika Kusini.

Rwanda inaongoza kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi za Afrika Mashariki ikifuatiwa na Kenya yenye wagonjwa 42, Uganda 33 na Tanzania 13.

Hata hivyo, mpaka sasa mataifa ya Burundi na Sudan Kusini hayajarekodi maambukizi ya virusi vya corona.

Jumamosi iliyopita Serikali ya Rwanda ilianza kugawa msaada wa chakula kwa familia zisizojiweza na ambazo zimeathiriwa na amri ya kukaa nyumbani.

Wiki iliyopita Rwanda ilitangaza kufunga mipaka yote ya nchi hiyo na watu kuamrishwa kusalia majumbani mwao katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na watumishi wote wa serikali na wa kibinafsi kufanyia kazi nyumbani na safari za kuenda mikoani kusitishwa kwa wiki mbili huku usafiri wa bodabobda ukisitishwa.