Wanafunzi wa Chuo Kikuu Makerere wavamia kituo cha polisi

Muktasari:

  • Jumatatu iliyopita wanafunzi 15 walikamatwa walipokuwa wakijaribu kuandamana kuelekea katika ofisi ya Rais Yoweri Museveni kushinikiza kupunguzwa gharama za masomo.

Kampala, Uganda. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda wamevamia kituo cha polisi wakishinikiza kuachiliwa huru kwa wenzao 15 waliokamatwa.

Jumatatu iliyopita wanafunzi hao walikamatwa baada ya kufanya maandamana wakipinga ongezeko la karo ya masomo iliyoidhinishwa mwaka jana.

Jana Jumatano Oktoba 23 wanafunzi hao walivamia na kukizingira kituo cha Polisi cha Wandegeya kilichopo jijini Kampala ambako inadaiwa wanafunzi wenzao wanashikiliwa.

Waafunzi hao walianza kwa maandamano yaliyoanzia shuleni kwao mpaka kituoni hapo huku wakishika mabango yaliyokuwa yameandikwa maneno ya kushinikiza kuachiwa kwa wenzao.

Gazeti la The Daily Monitor la Uganda lililiandika kuwa tukio hilo lilisababisha kusimama kwa muda kwa shughuli kituoni hapo mpaka pale viongozi wa jeshi hilo walipozungumza na wanafunzi hao na kuwasihi kurejea shuleni. Baadaye wanafunzi hao walikubali kurejea shuleni.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wanafunzi hao walikamatwa walipokuwa wakijaribu kuelekea katika ofisi ya Rais Yoweri Museveni ili kumuomba aingilie kati mzozo huo.

Picha zilizotumwa kwenye mtandao wa Twitter zilionyesha wanafunzi hao wakikamatwa na askari wa Jeshi la Uganda kwa kushirikiana na polisi wakiwa nje ya lango la chuo hicho.

Mwishoni mwa mwaka jana uongozi wa chuo hicho ulitangaza ogezeko la karo ya masomo jambo lilopingwa na wanafunzi na kuendesha maandamano kwa lengo la kushinikiza kupunguzwa kwa ada hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na kijamii nchini humo na kuwataka wasimamizi wa vyuo vikuu kutafuta njia za kuhakikisha wanapata fedha za kuendesha shule ili kupunguza maandamano kama hayo.