Watoto 11 waambukizwa corona Uganda

Muktasari:

Uganda sasa ina jumla ya watu 44 walioambukizwa virusi vya corona.

Kampala, Uganda. Idadi ya maambukizi ya corona imeongezeka nchini Uganda baada ya watoto 11 kuthibitika kuwa na virusi hivyo.

Akitangaza maambukizi mapya jana Jumanne Machi 31, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema watoto hao wanakwaya maarufu nchini humo.

Rais Museveni alisema watoto hao wanatoka katika kwaya ya ‘Watoto Children's Choir’ ambayo mara kwa mara husafiri nje ya nchi.

“Wagonjwa wote walikuwa katika karantini baada ya kurejea kutoa nje ya nchi. Baada ya kupimwa wote waligundulika wameathirika na corona,” alisema Rais Museveni.

Rais Museveni alisema mara nyingi kwaya hiyo hutumbuiza katika nchi za Marekani, Canada na Uingereza.

Alisema wagonjwa hao wapya wanafanya idadi ya walioambukizwa virusi hivyo nchini Uganda mpaka jana jioni kufikia 44.