Watoto 5,000 wafa kwa surua DRC

Friday November 22 2019

Ugonjwa surua umewaua watoto takriban 5,000 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mwaka 2019, kulingana na taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kulungana na taarifa hizo, karibu watoto 250,000 wameambukizwa ugonjwa huo mwaka huu pekee.

Shirika la afya duniani WHO linasema kuwa ugonjwa huo ndio janga linalosambaa kwa kasi mno katika nchi hiyo ambayo pia inasumbuliwa na ugonjwa wa Ebola.

Surua katika DRC imeua idadi ambayo ni mara mbili ya wagonjwa waliofariki kutokana na Ebola katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.

Tayari Serikali ya DRC kwa ushirikiano na WHO imezindua chanjo ya dharura ya surua tangu Septemba, inayowalenga watoto 800,000.

Kwa mujibu wa BBC, miundombinu mibaya ya usafiri, mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, na ukosefu wa tiba za mara kwa mara, vimekuwa vikwazo  vya juhudi za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.

Advertisement

Tayari watoto milioni nne wamepewa chanjo ya surua, lakini wataalamu wameonya kwamba idadi hiyo ni chini ya nusu ya watoto wote nchini humo wanaohitaji chanjo hiyo ambayo hazitoshi.

Surua ni virusi vinavyosababisha mtoto kuwa na mafua na kupanda mara kwa mara kwa joto mwilini. Baadaye mgonjwa hupata vipele kuanzia usoni na kusambaa mwilini.

Pamoja na kwamba wagonjwa wengi hupona, surua inaweza kusababisha ulemavu wa muda mrefu na hata kifo.

Inakadiriwa kwamba jumla ya watu 110,000 duniani hufariki kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.

Advertisement