Watu saba wauawa katika mlipuko wa gari, Kabul

Wednesday November 13 2019

 

Kabul. Takribani watu saba wameuawa na wengine saba kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu lililotegwa kwenye gari jana majira ya asubuhi, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani amethibitisha.

Msemaji huyo, Nasrat Rahimi amesema bomu hilo lililipuka maeneo ya jirani na ilipo wizara ya mambo ya ndani na kaskazini mwa Uwanja wa Ndege wa Kabul.

Amesema waliopoteza maisha wote walikuwa ni raia “hizi ni taarifa za awali, taarifa za kina tutazitoa baadaye,” alisema Rahimi.

Chanzo cha habari katika wizara ya mambo ya ndani kimesema kilisababishwa na mtu mmoja aliyejitoa mhanga katika gari hilo na kwamba alikuwa amelenga msafara wa magari ya serikali katika barabara kuu.

Mlipuko huo ulitokea siku moja baada ya Rais wa nchi hiyo, Ashraf Ghani kutangaza kwamba serikali itawaachia huru wafungwa watatu wa kundi la Taliban katika mpango wa kubadilishana wafungwa na mateka kutoka nchi za Magharibi walioshikiliwa na vikundi vya kigaidi mwaka 2016.

Wafungwa watatu wa Taliban ni pamoja na Anas Haqqani ambaye alikamatwa mwaka 2014 na ambaye kaka yake ni naibu kiongozi wa Taliban na mkuu wa mtandao wa Haqqani, washirika hatari wa Taliban.

Advertisement

Ghani hakufafanua hatma ya mateka wa Magharibi—kutoka Australia na Marekani, wote ni maprofesa katika Chuo Kikuu cha America cha Kabul, na haikuwa wazi lini na wapi wataachiwa huru.

Ghani alisema uamuzi huo utasaidia “kutengeneza njia” ya kuanza kwa mazungumzo yasiyo rasmi kati ya serikali na Taliban ambao kwa muda mrefu wamekataa kujadiliana na serikali ya Kabul.

SOMA ZAIDI

Advertisement