Watu wanane wafa kwa kushambuliwa na risasi Ujerumani

Muktasari:

Ni baada ya mtu mwenye silaha kufyatulia risasi za moto usiku wa manane katika klabu ya shisha.

Ujerumani. Mwanaume mmoja nchini Ujerumani amewaua kwa risasi watu wanane waliokuwa katika klabu mbili tofauti za shisha.

Matukio hayo yalitokea usiku wa kuamkia jana katika mji wa Hanau ulipo katika Jimbo la Hessen, Mashariki mwa jiji la Frankfurt.

Aidha, katika matukio hayo mwanaume huyo pia aliwajeruhi watu wengine watano.

Polisi nchini Ujerumani ilisema kuwa mwanaume huyo alitekeleza matukio hayo kwa nyakati tofauti kati ya saa saa 4.00 na 7.00 usiku.

Hata hivyo, mwanaume huyo alikutwa amekufa saa chache baada ya kutekeleza uharifu huo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, mwili wa mtuhumiwa huyo ulikutwa nyumbani kwake saa 11.03.

Wakizungumzia tukio hilo, polisi walisema mtuhumiwa huyo awali alivamia katika baa moja iliyopo katikati mwa jiji huo na kufyatua risasi ovyo zilizosababisha vifo vya watu watatu.

“Baadaye alikimbia na kwenda katika baa nyingine iliyopo katika kitongoji cha Hanau Kesselstadt na kuua watu wengine watano,” ilisema taarifa hiyo ya polisi.

Kwa mujibu wa polisi, haijajulikana sababu ya mauaji hayo na kwamba uchunguzi umeanza mara moja.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Can-Luca Frisenna anayefanya kazi katika moja ya baa hizo alisema baba yake na kaka yake walikuwa katika eneo hilo wakati shambulio hilo lilifanyika.

“Ilikuwa kama filamu, hakuna aliyeamini lakini watu walikufa, Frsenna aliliambia shirika la Reuters.

Shambulio hili linakuja siku nne baada ya shtaka lingine huko Berlin, karibu na onyesho la ucheshi la Uturuki kwenye ukumbi wa tamasha la Tempodrom, ambalo lilimuua mtu mmoja.