Waziri, gavana Somalia wajeruhiwa na al- Shabab

Muktasari:

Shambulio hilo lilifanywa katika Jimbo la Puntland lenye utawala wake wa ndani nchini Somalia na kuwahusisha viongozi hao waliokuwa katika gari.

Khartoum, Somalia. Waziri wa Mambo Ndani nchini Somalia, Mohamed Abdirahman na Gavana wa Jimbo la Puntland, Abdisalan Hassan Hersi wamejeruhiwa katika shambulio la kigaidi.

Viongozi hao pamoja na kamanda wa zamani wa polisi na raia mmoja nao pia walijeruhiwa kwenye mashambuo hilo.

Shambulio hilo la kujitoa muhanga lilitokea Jumapili iliyopita Machi 19, linadaiwa kutekelezwa na kundi la al-Shabab katika Mkoa wa Nugaal, Somalia

Watu waliokuwa karibu na neo hilo walisema walisema walishuhudia mwanaume mmoja akijirusha mbele ya gari walilokuwa viongozi hao na kulipuka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi nchini Somalia, mtu huyo aliyekuwa amejivisha mabomu hakufahamika mara moja.

Taarifa hiyo ilisema watu wote waliokuwa katika gari hiyo walijeruhiwa vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa Nugaal kwa matibabu.

Muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo, kundi la al-Shabab lilitoa taarifa ya kuhusika na shambulio hilo.

Kwa miongo kadhaa kundi la al-Shabaab limekuwa likitekeleza mauaji nchini Somali ambako mwaka 2011 Jeshi la nchi hiyo lilitangaza kuondoa ngome yake katika mji mkuu wa Mogadishu.

Hata hivyo, kundi hilo bado linadhibiti maeneo makubwa nje ya Mogadishu na mara kwa mara limekuwa likifanya mauaji ya watu katika maeneo ya mikusanyiko, hoteli na usafiri wa umma.