Waziri Mkuu wa Israel awekwa karantini

Israel. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na wasaidizi wake wa karibu wamewekwa karantini baada ya mfanyakazi katika ofisi yake kupimwa na kukutwa na virusi vya ugonjwa wa corona.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 70, imeeleza kuwa uamuzi wa kumuweka karantini ni kwa lengo la kuchukua tahadhari tu, kwasababu hata hivyo kiongozi huyo hajahusiana wala kugusana na mfanyakazi huyo mwenye maambukizi ya Covid-19
Taarifa zimeeleza kuwa kwa uchunguzi wa awali uliofanyika, ulionyesha hakukuwa na haja ya kumuweka karantini kutokana na kutogusana na mgonjwa huyo.
Vilevile, imeelezwa kuwa kwa wiki mbili zilizopita kiongozi huyo na mfanyakazi wake hawakuwahi kuwa kwenye chumba kimoja kwa wakati mmoja.
Israel imesema kiongozi huyo kwa takriban wiki mbili alikuwa akitimiza majukumu yake na vikao kwa njia ya mtandao na video.