Waziri Mkuu wa Itali ajiuzulu

Muktasari:

Katika hotuba yake Waziri Mkuu, Giuseppe Conte amemshutumu kiongozi huyo wa upinzani kwa uweka maslahi binafsi na ya chama chake mbele badala ya Taifa.

Itali.  Waziri Mkuu wa Itali, Giuseppe Conte ametangaza kujiuzulu nafasi yake baada ya Serikali yake kutoungwa mkono.

Waziri Conte alitangaza uamuzi huo jana Jumanne Agosti 20 na kuwaambia wabunge wa nchi hiyo kwamba anajiuzulu kwa sababu kiongozi wa chama cha upinzani cha Ligi, Matteo Salvini ameamua kuondoa uungaji mkono kwa Serikali anayoiongoza.

Baada ya tangazo hilo bungeni, Waziri Mkuu Conte alisema   atakwenda kumfahamisha rasmi Rais wa Itali, Sergio Mattarella juu ya uamuzi wake.

Hata hivyo, Rais Mattarella anaweza kukubali uamzi huo au kumuomba waziri Conte kuendelea kuwapo katika Serikali hiyo.

Endapo atakubaliana na uamuzi wa kujiuzulu kwake Rais Mattarella anapaswa kushirikana na viongozi wengine kupata namna ya kuunda Serikali nyengine ya muungano na ikishindikana anapaswa kuvunja Bunge na kuwa na uchaguzi mpya Oktoba, mwaka huu.

Katika hotuba yake waziri Conte alimshutumu kiongozi huyo wa upinzani kwa kuweka maslahi binafsi na ya chama chake mbele badala ya Taifa huku akionya kuwa hatua yake itaathiri uchumi.

Salvini ambaye ni kiongozi wa chama cha Ligi na naibu waziri mkuu wan chi hiyo ameonekana kujiongezea umaarufu katika kura ya maoni wakati wa malumbano ya miezi kadhaa juu ya maamuzi muhimu ya kisera na mshirika wake katika Serikali ya muungano.

Kiongozi huyo ambaye ameshaonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya uwaziri mkuu amekuwa akishinikiza kuitishwa kwa uchaguzi haraka.

Wiki mbili zilizopita kiongozi huyo wa chama cha Ligi nchini Italia alionesha nia yake ya kutaka kumalizika kwa Serikali ya muungano na kundi lisilopenda utawala la vuguvugu la nyota tano, baadae aliubadilisha uamuzi wake huo lakini kundi hilo likasema hatua yake imekuja kwa kuchelewa na hawawezi kurejesha mambo kama yalivyokuwa.

Kundi hilo sasa linatazamia kujaribu kuungana pamoja na chama cha upinzani cha Democratic na iwapo hilo halitowezekana basi Itali italazimika kuandaa uchaguzi huo mwezi Octoba au Novemba.