Waziri wa ulinzi aongoza urais Sri Lanka

Aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa

Muktasari:

Ni waziri wa zamani wa ulinzi aliyewabwaga wagombea wengine 32 akiwamo wa chama tawala na waziri wa makazi.

Colombo, Sri Lanka. Aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa anaongoza katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa urais na kumbwaga mgombea wa chama tawala.

Kura za awali zinaonyesha kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70 anaongoza kwa asilimia 52.87 na kufuatiwa na mgombea wa chama tawala na waziri wa makazi, Sjith Premadasa (52) aliyepata 39.67 kati ya kura zilizohesabiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya shirika la habari la Aljazeera, uchaguzi huo uliofanywa chini ya ulinzi mkali ikiwa ni miezi saba baada ya mashambulizi mabaya ya itikadi kali.

Rajapaksa, kiongozi mkuu wa upinzani alikuwa akishindana na wagombea wengine 32 walioshiriki kinyang'anyiro hicho.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Mahinda Deshapriya alisema karibu asilimia 80 ya watu milioni 15.99 waliosajiliwa kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo wa jana ambao ulikumbwa na matukio ya ghasia ambayo yalisababisha watu kadhaa kujeruhiwa.