Virusi vya corona vyaingia rasmi barani Afrika, vikiua zaidi ya 1,500

Muktasari:

Kisa cha kwanza cha virusi vya corona kimethibitishwa barani Afrika katika nchi ya Misri

Cairo, Misri. Hatimaye virusi vya ugonjwa wa corona (covic-19) vimethibitishwa kuingia barani Afrika.

Wizara ya Afya ya Misri, imethibitisha kutokea kwa mgonjwa wa kwanza katika nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo jana ilisema mgonjwa aliyebainika si raia wa Misri ingawa mpaka sasa hakufahamika ni wa nchi gani.

Kwa mujibu taarifa hiyo, maofisa wa afya wa Misri walimgundua mgonjwa huyo kupitia mpango wa kuwafuatilia abiria waliowasili kutoka chini ambazo zina virusi vya corona.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Misri, Khaled Megahed alisema serikali inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa huyo.

Megahed alisema hadi jana jioni hali ya mgonjwa hiyo ilizidi kuimarika tofati na alipogundulika.

“Kwa sasa mgonjwa huyo ametengwa katika eneo maalumu ili asiambukize wengine, atapatiwa matibabu kwa siku zote bila ndugu na jamaa zake kumkaribia,” alisema Megahed.

Alisema mamlaka zinazoshughulika na sekta ya afya nchini Misri zimeliarifu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusiana na mgonjwa huyo na taratibu zinaendelea ili kuhakikisha maambukizi hayo hayaendelei kusambaa kwa watu wengine.

Mapema mwezi huu Misri ilifuta safari zote za shirika la ndege ya taifa kwenda China.

Aidha, serikali ya nchi hiyo iliwaondoa raia wake 301 waliokuwa katika mji wa Wuhan ambao ni kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.

Mara baada ya wagonjwa hao kufikishwa nchini humo waliwekwa katika karantini kwa siku 14 ili wasiambukize watu wengine kisha kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Katika hatua nyingine, tajiri wa kwanza duniani, Bill Gates ameonya iwapo juhudi za makusudi hazitochukuliwa kudhibiti virusi vya corona barani Afrika hali itakuwa mbaya zaidi.

Tajiri huyo alisema iwapo virusi vya corona vitasambaa barani Afrika hali itakuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo nchini China.

Kwa sasa miji mbalimbali nchini China imefungwa kufuatia kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo.

Akizungumza jana mwanzilishi huyo wa kampuni ya kompyuta ya Microsoft alisema ingawa bado kuna mengi yasiyojulikana kuhusu virusi hivyo lakini ni dhahiri kwamba vitasababisha janga kubwa iwapo vitasambaa katika mataifa ya Kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na bara la Asia.

Kufuatia kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo, mfuko wa fedha kwa ajili ya kutoa misaada unaoendeshwa na Bill Gates pamoja na mke wake Melinda, umechangia dola milioni 100 ili kupambana na mlipuko huo pamoja na kutafuta chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Wakati huo huo, zaidi ya watu 1,500 wamefariki dunia mpaka jana mchana kutokana na virusi vya corona.

Aidha, zaidi ya watu 66,000 wameshaambukizwa virusi hivyo nchini China, vilivyoanzia katika Jimbo la Hubei katika mji wa Wuhan miezi mitatu iliyopita na kusambaa katika nchi zaidi ya 27 duniani.

Tume ya Afya ya China imewataka watu wote wanaorejea katika mji mkuu wa Beijing kufuatia kipindi cha mapumziko kubaki majumbani mwao kwa siku 14 kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi hayo.

Nchi kadhaa zimepiga marufuku ya kuwasili kwa raia wa China na baadhi ya mashirika makubwa ya ndege yamesimamisha huduma zao nchini humo.

Ijumaa iliyopita, Rais wa China, Xi Jinping alikiri kwamba mlipuko huo umedhihirisha mapungufu katika mfumo wa kukabiliana na dharura ya afya nchini humo na kuahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo.