Virusi vya corona Corona yabisha hodi Ufaransa

Muktasari:

Virusi vya Corona vinavyoisumbua China vimethibitika kuingia nchini Ufaransa ambako mpaka jana watu watatu wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo.

Paris, Ufaransa. Serikali ya Ufaransa imethibitisha kuwapo kwa maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Ufaransa ilisema hadi kufikia leo asubuhi watu watatu walithibitika kuwa na ugonjwa huo ulioanzia China.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wagonjwa wawili walipatikana katika mji mkuu wa Paris na mmoja alitokea mji wa Bordeaux.

Taarifa hiyo ilisema kwa sasa mamlaka za afya nchini humo zinajaribu kubaini watu wengine waliokuwa na maingiliano na wagonjwa hao waliambuklizwa virusi hivyo.

Aidha, Wizara ya Afya nchini humo iliwasisitiza wananchi wote kutoa taarifa ya kuwapo kwa wagonjwa wenye dalili kwa mamlaka husika ili kufanyiwa uchunguzi haraka.

Katika hatua nyingine, mgonjwa wa pili mwenye virusi vya corona amegndulika nchini a Marekani Ijumaa iliyopita.

Wakati huo huo, mataifa kadhaa ya Afrika yameanza upimaji wa joto la mwili katika viwanja vya ndege na kuchukua hatua za tahadhari kuzuia kusambaa kwa virusi vipya vya Corona.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilisema kuwa inachukua hatua za tahadhari katika viwanja vya ndege na bandari zikiwalenga watu wanaotoka mataifa yaliyoathirika na virusi hivyo.

Nigeria, Uganda, Ghana na Shelisheli pia zimetangaza mipango ya kuchukua hatua kama hizo kukabiliana na virusi vya corona ambako wasafiri watapimwa joto la mwili kubaini dalili za maambukizi hayo.

Kwa upande wake, taasisi ya magonjwa ya mripuko nchini Afrika Kusini ilisema bado haijaweka mifumo ya kupima watu kwenye maeneo ya kuingia nchini humo lakini imewataka raia wote waliokuwa China hivi karibuni kufanya uchuguzi wa afya.