Mkapa asema hakupenda kutukuzwa

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Dar es Salaam. Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema hakupenda kutukuzwa katika kipindi cha utawala wake na katika kudhihirisha hilo aligomea mambo mawili; kuitwa mtukufu na sura yake kuwekwa kwenye fedha.

Sifa hiyo ya mtukufu haitumiki katika anga za siasa isipokuwa neno “mheshimiwa” huku fedha za nchi zikiwa na picha ya muasisi wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere pamoja na michoro ya rasilimali.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” kilichozinduliwa wiki hii, Mkapa ameeleza sababu za kuchukua uamuzi huo.

Rais huyo mstaafu alisema alipiga marufuku kuitwa “mtukufu” kwa kuwa hakutaka kutengeneza mazingira ya ukuu dhidi ya wananchi wengine.

Mkapa anaelezea kuwa alipenda kuitwa “mheshimiwa” sawa na mawaziri, wabunge na wakuu wa mikoa.

“Nilizuia kuitwa mtukufu kwa sababu sikupenda kujikweza kama mtu mwenye nguvu zaidi katika nchi,” anasema Mkapa, ambaye kazi yake ya kwanza kwenye utumishi wa umma ilikuwa ni Bwana Shauri mwaka 1961 mjini Dodoma.

Amesema pia alikataa kuitwa “mtukufu” kwa kuwa aliona kitendo hicho kinaweza kuwagawa Watanzania.

Mkapa, ambaye alikuwa Rais kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, anasema alizingatia hilo kwa kuwa nchi ilikuwa inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“Niliamini Tanzania ilikuwa bado nchi changa halafu nianze kujiweka juu ya wengine, niliona halikuwa jambo sahihi pia kipindi naingia kwenye urais tulikuwa tupo kwenye miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi ya siasa,” anaeleza Mkapa.

Mkapa aliingia Ikulu katika uchaguzi wa mwaka 1995, ukiwa wa kwanza wa vyama vingi tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.

Msafara mdogo

Mkapa pia anaeleza kuwa hakupenda msafara wake kuwa na magari mengi pamoja na mbwembwe za pikipiki.

“Hii habari ya kuwa na magari mengi kwenye msafara wangu kwa kweli sikupendelea. Niliamini hali hiyo ilikuwa inaleta picha isiyo nzuri kwa watu niliokuwa nawaongoza,” anasema Mkapa.

Mkapa anasema alikuwa anapenda misafara yake iwe na magari machache na bila ya mbwembwe.

Mkapa anagusia pia suala la ulinzi wake, akisema katika kipindi chake alipenda awe na ulinzi usiotoa taswira ya kutisha watu.

Anadai alifahamu fika kuwa kutokana na kuwa Amiri Jeshi Mkuu, usalama wake ulikuwa jambo nyeti lakini alipendelea ufanyike katika hali ambayo haitoi picha kuwa ni mtu tofauti na wengine.

Mkapa anasema alikuwa hapendi kuona ulinzi wake ukijumuisha askari wengi wenye magwanda.

“Nilikuwa napata shida sana na hasa nikienda ziara za mikoani kuona askari wenye magwanda wamejaa sehemu nilipokuwa. Sikupenda hali ile maana niliona kama najiweka mbali na watu,” anaeleza Mkapa.

Kisa cha kukataa sura yake kwenye pesa

Kiongozi huyo alisema katika kipindi cha miaka 10 alichoishi Ikulu, kulifanyika mabadiliko ya fedha mara mbili. Ni katika kipindi hicho pia Benki Kuu ya Tanzania ilitoa noti za Sh5,000 na Sh10,000.

Mkapa anasema aliweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza kwa sura yake kutowekwa kwenye fedha.

Mabadiliko hayo yalifanyika mwaka 1997, wakati ilipoondolewa picha ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na badala yake ikawekwa picha ya twiga.

Anasema alichukua uamuzi huo kutokana na tabia yake ya kutopenda kujichukulia kuwa mtu muhimu kuliko wengine.

Hata hivyo, aliona lilikuwa jambo zuri zaidi kwa picha za waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume, zitumike kwenye fedha.

Anaeleza pia alichukua uamuzi huo ili kuepusha gharama za kubadilisha noti na sarafu kila mara.

Mkapa, ambaye anasifika kuwa alifanya kazi kubwa ya kufufua uchumi na kurejesha imani kwa mataifa wahisani, anaeleza kuwa aliamiani suala hilo lingesumbua kuwa kila utawala unapobadilika na fedha zinabadilishwa.

Tanzania lianza kutumia fedha yake yenyewe mara ya kwanza mwaka 1966, kabla ya hapo ilikuwa inatumia fedha moja na nchi za Kenya na Uganda.