MUUNGANO TANGANYIKA- ZANZIBAR 1964: Nyerere aanza kupigia upatu umoja A.Mashariki -2

Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona jinsi viongozi wa nchi za Afrika walivyotoa rai ya kutaka Afrika iwe na sauti moja katika kusaidia nchi ambazo zilikuwa hazijapata uhuru wakati walipokutana jijini Addis Ababa, Ethiopia. Lakini haikuwa rahisi kutekeleza yale waliyokubaliana kutokana na mazingira tofauti. Nchini Tanganyika, Rais Julius Nyerere alikuwa na mkakati tofauti kuanza kutimiza kile walichokubaliana, lakini mataifa ya Magharibi nayo yalikuwa na mipango yao.

Wakati viongozi wa Afrika wakimaliza kikao chao jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa wito wa kushirikiana kutokomeza ukoloni na pengine kuunda Afrika moja, mazingira hayakuwa kama walivyotarajia. Katika nchi za Tanganyika na Zanzibar, robo ya kwanza ya mwaka 1964 ilikuwa na matukio mengi kwa siasa kuliko wakati mwingine wowote. Pamoja na maazimio ya Addis, Mwalimu Julius Nyerere alianza na harakati za kuzifanya nchi za Afrika Mashariki kuwa shirikisho kuanzia mwishoni mwa Machi hadi Aprili 1964. Lakini hadi kipindi hicho inaonekana hakuwa na wazo la kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar.

Hata mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar na maasi ya kijeshi Tanganyika, hakukuwa na wazo la muungano wa pande hizo mbili. Kilichokuwa kikizungumzwa katika kipindi chote ni Shirikisho la Afrika Mashariki, ambalo baadaye halikufanikiwa, wajumbe wa mkutano wa kuanzishwa shirikisho hilo waliokutana mjini Nairobi, Kenya walimaliza mkutano wao kwa kutoelewana.

Mawazo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yalikuja karibu juma moja tu baada ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo ya kuanzisha shirikisho la Afrika Mashariki uliofanyika Aprili 11, 1964 mjini Nairobi.

Siku tano baadaye, Mwalimu Nyerere aliingia ofisi za gazeti la chama cha Tanu, The Nationalist and Freedom alikoalikwa kuzindua na kutazama maandalizi ya toleo la kwanza la gazeti hilo ambalo lingetoka kwa mara ya kwanza siku iliyofuata.

Alipoonyeshwa kielelezo cha gazeti hilo, alimuita msaidizi wake aliyeongozana naye, Rashidi Kawawa na kumuonyesha mojawapo ya vichwa vya habari vya gazeti hilo kilichoandikwa: “Maofisa wa Kenya watetea Shirikisho la Kenya, Tanganyika na Uganda”.

Ukweli ni kwamba maofisa hao hawakutetea shirikisho hilo kama ilivyoripotiwa gazetini, vinginevyo mkutano wa kuanzishwa shirikisho hilo usingevunjika mjini Nairobi. Angalau gazeti hilo lilisema kilichozungumzwa hadi Aprili 17 kuwa ni Shirikisho la Afrika Mashariki.

Zikiwa zimesalia siku tisa kabla ya muungano, gazeti hilo halikuzungumza habari yoyote ya Tanganyika kuungana na Zanzibar, na wala Shirika la Utangazaji la Tanganyika (Tanganyika Broadcasting Corporation, TBC) halikutangaza habari hizo. Inaelekea waandishi wa vyombo hivyo hawakujua lolote kuhusu muungano ambao ungezaa Tanzania. Na kama walijua, basi walifanya siri kwa maslahi fulani. Inavyoonekana ni kwamba hadi Aprili 17, Nyerere hakuwa amepata wazo la Muungano.

Au kama alikuwa nalo, hakulitilia maanani na wala hakuona kama lingewezekana. Pengine alilipata siku iliyofuata; pengine alipelekewa; pengine lilimjia katika ndoto, lakini akaitilia shaka ndoto hiyo. Vinginevyo ingejulikana kwa vyombo vya habari—hasa kwa gazeti kama The Nationalist and Freedom alilokwenda kulizindua.

Pamoja na Nyerere mwenyewe kutembelea ofisi za gazeti hilo na kuzungumza na waandishi wake, hakuwaambia mambo ya Muungano. Hata kwa kuwagusia tu. Aliridhishwa na habari kuu iliyozungumzia shirikisho la Kenya, Uganda na Tanganyika.

Siku hiyo Nyerere alimwambia Kawawa akisema: “Hili (The Nationalist) litakuwa kinara katika jitihada za Umoja wa Afrika.” Kawawa naye akatabasamu. Wakatabasamu pamoja. Jioni ya siku hiyo, Waziri Mdogo wa Mambo ya Ndani wa Tanganyika, Roland Mwanjisi akatumwa kwenda Kenya kueneza habari za gazeti hilo.

Siku iliyofuata, The Nationalist lilitolewa kwa mara ya kwanza na kusambazwa katika ofisi za Serikali. Waziri Mwanjisi aliwasili Kenya usiku uliotangulia na kuhutubia mkutano uliohusisha wabunge, maseneta na mabalozi wa Urusi na China—takribani watu 500—mjini Nairobi.

“Tunaamini The Nationalist litatoa mchango kwa Umoja wa Afrika—na Umoja wa Afrika Mashariki,” alisema.

Kilichozungumzwa na Waziri Mwanjisi ni “umoja wa Afrika na umoja wa Afrika Mashariki,” lakini si muungano au shirikisho la Tanganyika na Zanzibar.

Waziri wa Habari wa Kenya, Ramogi Achieng Oneko, alimuunga mkono Mwanjisi, akisema: “Gazeti hili linaweza, na litafanikiwa kuijenga sura ya Afrika katika Afrika Mashariki.”

Gazeti hilo lilizinduliwa wakati Tanganyika ikipita katika kipindi muhimu cha historia. Siku hiyo, Aprili 17, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zanzibar, Sheikh Abdulrahman Babu, alipiga marufuku utalii visiwani Zanzibar akisema amechukua hatua hiyo kwa sababu “kuna manowari za Marekani katika Pwani ya Afrika Mashariki” na kwamba amri hiyo “haitabadilika mpaka hapo manowari hizo zitakapoondoka”.

Kauli hiyo ilitolewa na Sheikh Babu siku moja baada ya kurejea kutoka Dar es Salaam alikoonana na Mwalimu Nyerere.

Babu aliaminika kama mtu ambaye alikuwa mwaminifu wa siasa za kikomunisti na amri yake ilitokana na meli ya taifa ambalo ni kinara wa ubepari kuwa pwani ya Afrika Mashariki. Hii iliashiria nini. Marekani walikuwa wanataka nini ukanda wa Afrika Mashariki?

Utafiti wa karibuni unaonyesha kuwa mbali na mazungumzo baina ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume kuhusu Muungano, inaonekana kulikuwa na harakati nyingine za kutaka pande hizo mbili kuungana kutokana na siasa za vita baridi ya dunia iliyokuwa imeshika kasi wakati huo.

Taarifa zinaonyesha kuwa mataifa ya Magharibi, hususan Marekani yalitaka kwa udi na uvumba muungano huo. Kulingana na kitabu cha Mwalimu: The Influence of Nyerere, nchi za Marekani, Uingereza, na Ujerumani Magharibi, ambazo Tanganyika ilizitegemea sana, zilikuwa na hamu ya kuona muungano huo kwa sababu kwa mtazamo wao kama Zanzibar ingeachwa, ingekuwa ‘Cuba’ ya Afrika, yaani ingekuwa ngome ya ukomunisti barani Afrika.

Katika mahojiano yaliyofanyika mwaka 1986 na aliyewahi kuwa balozi mdogo wa Marekani visiwani Zanzibar, na baadaye akawa mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) na hatimaye Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Frank Carlucci, alifichua kilichofichika katika akili yake.

Itaendelea kesho