‘Watoto wa ibilisi’ tishio

Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Thobias Mwilapwa  akizungumza wakati akifungua mkutano wa asasi za kiraia mkoa wa Tanga alipotangaza kutokomezwa kwa tishio la Ugaidi mkoani humo. BurhanI Yakub

Tanga. Kikundi cha vijana wanaojiita ‘Watoto wa ibilisi’ limekuwa tishio kwa maisha ya watu na mali zao baada ya kudaiwa kusababisha kifo cha mwenyekiti wa serikali ya mtaa na kujeruhi zaidi ya watu 10.

Hivi karibuni mwenyekiti wa mtaa wa Relini, Abdallah Mtiga aliuawa ikiwa ni takriban wiki moja tangu apishwe.

Hadi kufikia jana zaidi ya watu 10 walikuwa wametekwa, kuporwa na kujeruhiwa na kundi hilo wanaojiita ‘watoto wa ibilisi’ waliosambaa maeneo mbalimbali jijini Tanga.

Vijana hao wanadaiwa kutembea na panga, nyundo, misumeno na visu.

Akizungumza katika Baraza la Madiwani, mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku alieleza kuwa hali ni tete.

Mbaruku alisema vijana hao wanaojiita ‘watoto wa ibilisi’ hutembea kundi la zaidi ya watu 50 wakiwa na silaha mbalimbali.

“Hata familia yangu ni waathirika wa matukio hayo ya kundi hili,” alisema.

Naye meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapha maarufu Seleboss alisema kuibuka kwa kundi hilo siyo tishio tu kwa wananchi, bali hata kwa viongozi wamo hatarini na kutaka mkuu wa wilaya kutoa tamko kwenye baraza hilo.

“Kutokana na hali ya usalama ilivyo tete nataka nipewe ulinzi kwa ajili ya usalama wangu, kabla ya kwenda msikini kila siku nafanya mazoezi alfajili kwa hali hii nitakuja kutekwa,” alisema Mustapha.

Akizungumzia suala hilo, mkuu wa wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa licha ya kukiri uwapo wa kundi hilo lililosababisha kifo cha kiongozi huyo, aliwataka wananchi na viongozi kutokuwa na hofu juu ya usalama wao na mali zao kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza kuchukua hatua na baadhi wamekamatwa.

Mwilapwa alitaja hatua hizo kuwa ni kuimarisha doria mitaani na kufanikisha kuwakamata baadhi ya vijana ambao walitajwa na wenzao.

Hata hivyo, Mwilapwa alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu ili hatua kali zichukuliwe.

Katika hoja nyingine iliyoibuliwa ni wizi wa mali kwenye majengo ya umma zikiwamo shule na zahanati, unaofanywa na vibaka kutokana na maeneo hayo kukosa ulinzi.

Hoja hiyo ilitolewa na diwani wa Duga, Khalid Rashid alisema wizi wa mali za shule unaofanywa na vibaka majengo hayo ni kutokana na kukosa ulinzi.

Aliitaka halmashauri ihakikishe inaweka ulinzi maeneo hayo ili kudhibiti hali hiyo, kwani Serikali inapata hasara. “Tusisubiri mali za umma ziishe halafu ndiyo tuanze kupaza sauti, tuimarishe ulinzi maeneo hayo kwa sababu kinachofanyika ni kusababisha wananchi wapate shida iwapo miundombinu hiyo itaendelea kuibwa, ni wazi shule na zahanati zitafungwa,” alisema.