ACT yamkingia kifua Zitto

Zitto Kabwe

Dar es Salaam. Uamuzi wa Benki ya Dunia (WB) kuzuia kwa muda mkopo wa Dola 500 milioni za Marekani zinazotakiwa kuboresha elimu, umeendelea kuchukua sura mpya baada ya ACT-Wazalendo kusema inafuatilia kwa karibu ambacho Zitto Kabwe anakipitia kwa sasa.

ACT-Wazalendo ilitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja tangu Spika Job Ndugai kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi kuangalia kama alichokifanya Zitto kina jinai.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa ACT-Wazalendo, anatuhumiwa kuiandikia barua WB Januari 22 kuitaka isitoe mkopo wa masharti nafuu kutokana na Tanzania kutotekeleza baadhi ya masuala, elimu na kijamii.

Juzi, Ndugai alitoa wito huo kwa Profesa Kilangi baada ya mjadala uliotokana na hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel aliyetaka Zitto achukuliwe hatua kwa kitendo hicho.

Katika maagizo yake, Ngudai alisema baada yaAG kupitia ataangalia kama kuna jinai na atachukua hatua.

Jana, Katibu wa Uenezi wa ACT, Ado Shaibu aliliambia Mwananchi kuwa alichokifanya Zitto kina baraka za chama hicho.

Ado alisema anawashangaa baadhi ya wabunge wanaozungumza maneno ya kumbeza Zitto, kwani uhalisia alipaswa kupongezwa kwa kutimiza wajibu wake wa kibunge.

“Zitto amefanya kazi ambayo ilipaswa kufanywa na wabunge wote, ameisimamia Serikali ni mtu wa kupongezwa. Kuhusu kutumia nembo za Bunge ana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa ni mbunge halali,” alisema.

Alisema sababu alizozitoa Zitto WB ziko wazi na hakuna mwenye uwezo wa kuzipinga, lengo lake ni kupigania usawa wa elimu kuhakikisha watu wote wanasoma na mimba isiwe kikwazo.

Pia, Ado alisema ngome ya wanawake ya chama hicho itatoa msimamo juu ya hatua hiyo ya benki na ACT inafuatilia kwa karibu kauli za vitisho anazopewa kiongozi wake.

Alisema endapo kiongozi huyo ataendelea kupokea vitisho chama kitatoa msimamo juu ya hilo.

Katika barua ya Zitto anaitaka WB kutokuidhinisha mkopo huo kwani kuna masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini, ikiwamo wanasiasa wa upinzani kuzuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa.

Zitto anaieleza benki hiyo kwamba Februari 3 hadi 6 atakuwa Washington DC nchini Marekani atakuwa tayari kwenda kutoa ufafanuzi zaidi wa suala hilo.