AG aanza mikakati kushughulikia kesi za uchaguzi 2020

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi

Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi amewataka mawakili wa serikali kujipanga kuzishughulikia kesi za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ipasavyo.

“Kwa uzoefu nilionao inaonyesha kuna kesi nyingi zinafunguliwa mahakamani wakati wa uchaguzi, kabla na baada ya uchaguzi hivyo, kwa kutumia baraza hili mjiandae kikamilifu kuzishughulikia na kuivusha nchi salama katika uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani na hata baada ya uchaguzi,” alisema Kilangi, wakati akifungua kikao cha kwanza cha baraza la wafanyakazi ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Aliwaeleza kuwa wana jukumu la kuiwakilisha serikali katika uchaguzi huo hivyo wajiandae kikamilifu kuhakikisha wanaivusha nchi salama na kuongeza kuwa mawakili hao wamewawakilisha vyema katika kesi ziilizofunguliwa ndani na nje ya nchi katika kudai na kuleta haki.

Aidha alisema nchi inapoelekea katika uchumi wa kati na viwanda, inazalisha kesi nyingi ambazo huharibu ama kurudisha nyuma maendeleo na kulitaka baraza hilo liwe chachu ya kuendeleza mapambano kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Ni wajibu wenu kuendelelea kufanya kazi kwa bidii, ubora na ufanisi licha ya kuwepo kwa changamoto na kuongeza kama nchi tunakwenda vizuri katika kila nyanja yanapotokea haya siyo wote wanafurahi hasa wale ambao maslahi yao yameguswa ama mirija yao imekatwa na hapa ndiyo utawajua marafiki na wasio marafiki.

“Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali ni muhimu sana katika nchi hii kwa sababu masuala yote ya kesi tunawatazama nyie na masuala yote ya sheria tunaitazama ofisi ya mwanasheria mkuu pasipokuwa na ufanisi mtaiangusha nchi.” alisema Profesa Kilangi.

Pia alitoa wito kwa wafanyakazi kuacha kutumia fursa za vikao kujadili maslahi yao, bali wajadili namna za kuboresha na kuongeza ufanisi katika shughuli zao ili kuleta maendeleo nchini.

Aliwaeleza kuwa ili kuifikia Tanzania yenye uchumi wa kati na viwanda ni lazima kuwepo na uwazi katika uwajibikaji wao na wafanye kazi kwa ubora na ufanisi zaidi.

Alibainisha kuwa kumekuwepo na changamoto ya kutokuwepo kwa takwimu sahihi za mashauri ya madai ambayo serikali inashtakiwa.

“Hakuna takwimu sahihi kwa sababu utunzaji wa kumbukumbu una dosari kwa siku zilizopita hivyo ni lazima waboreshe na kuzingatia utaratibu wa serikali,” alieleza Profesa Kilangi.

Kwa upande wa Wakili Mkuu wa Serikali, Clement Mashamba alisema ndani ya miaka miwili toka ofisi hiyo ianzishwe wameiwakilisha serikali katika mashauri zaidi ya 2,000 ndani na nje ya nchi na kwamba wiki hii wamepelekewa mashauri matatu ya kuiwakilisha nchi.

Alisema wanaendelea kuboresha huduma ila changamoto inayowakabili ni namna ya kuwa na mfumo wa kielektroniki ilikuwa na takwimu sahihi za mashauri.

Alibainisha pia kuwa ipo haja ya kujenga masjala ya kisasa ya kisheria itakayokuwa na kesi zenye maslahi ya kiuchumi na kisiasa zilizofunguliwa dhidi ya Serikali ili kujua idadi ya kesi walizonazo

Hata hivyo alisema wanaendelea kuboresha miundombinu licha ya kuwepo kwa changamoto ya kutokuwepo na ofisi na vitendea kazi mikoani.