Aliu: Familia ya watoto watano wanaotamba katika udaktari

Unaweza kufikiri ni simulizi tu pengine ya kusadikika. Lakini ni uhalisia.

Tujikumbushe. Unaikumbuka familia ya Matumla iliyosheheni wanamasumbwi ikiongozwa na Rashid Matumla aliyetamba ndani na nje ya nchi?

Ni hivi. Kama masumbwi yalivyotawala kwa kina Matumla ndivyo taaluma ya udaktari ilivyovuta kiti na kuweka makazi katika familia ya Aliu iliyoko kaskazini mwa Nigeria.

Alianza Salamat kusomea udaktari wa mifumo ya fahamu, wakafuatia nduguze wanne ambao ni Raliat, Khadijah na Medinah.

Yeye na wenzake hawakujali vikwazo vilivyopo katika jamii nyingi za Kiafrika, ambavyo vimekuwa vikiwaweka kando watoto wa kike katika elimu. Walipofikia ni kielelezo cha kile wanachoweza kukifanya wazazi na hata watoto wenyewe katika masomo.

Katika orodha hiyo ya watoto watano, kuna daktari wa upasuaji, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na uzazi, daktari wa famila na masuala ya afya ya jamii.

Kudhihirisha kuwa familia hii imebarikiwa, imeweza kutoa daktari bingwa wa kwanza mwanamke katika nchi za Afrika Magharibi.

Salamat Aliu ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kwa ukanda wa Afrika Magharibi kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu. Na huyu ndiye aliyefungulia mlango wenzake kuingia kwenye fani adhimu ya udaktari.

Waanza kujulikana

Awali hakuna aliyekuwa akiifahamu hiyo familia lakini nguvu ya teknolojia imefanya sasa mijadala mingi baada ya Dk Halima ambaye ni mtoto wa kwanza kwenye familia hiyo kuweka mtandaoni picha iliyomuonyesha akiwa na wadogo zake.

Si ajabu mtu kuweka picha akiwa na ndugu zake lakini hii iliyowekwa na Dk Halima ilikuwa na ujumbe mzito ikiwaonyesha wanafamilia hao wote wakiwa na sare za udaktari.

Nyuso za tabasamu za wanasayansi hawa zilipamba picha hiyo na kusindikizwa na maneno ya kutia moyo yaliyoandikwa na Dk Halima katika akaunti yake ya twitter.

Maneno hayo yanasomeka: “Kwa wadogo zangu, rafiki zangu wa karibu na wenzangu katika taaluma ya tiba. Raliat, Salamat, Khadijah na Medinah najivunia kuwa na uhusiano wa damu na nyie. Siwezi kuomba ndugu bora zaidi yenu.’’

Anaongeza: ‘’Mmeifanya safari ya maisha kuwa rahisi, kujaliana, kutiana moyo na kuinuana mmoja anapoanguka ndiyo maisha yetu.Tumepitia vikwazo vingi kwa pamoja. Nawapenda sana. Tumewafanya wazazi wetu wajivunie,”

Inawezekana

Kilichotokea kwa familia ya Aliu kinaweza kutokea kwenye familia yoyote hapa nchini, endapo wazazi watawekeza kwenye elimu na watoto wataweka kipaumbele kwenye elimu huku watoto nao wakiamini katika kutimiza ndoto zao.

Ni wakati sasa kwa jamii kuondoka na ile dhana kwamba elimu haina maana kwa mtoto wa kike.

Septemba mwaka 2019 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akiwa wilayani Itilima alitoa ujumbe mzito kwa wazazi kuhusu kuwasomesha watoto wa kike.

Naibu waziri huyo aliwataka wazazi kuacha kuwageuza mitaji watoto wao wa kike kwa kuwaozesha mapema na badala yake wawasaidie katika kupata elimu ili baadaye wawe msaada kwao na taifa kwa ujumla.

“Niwaambie kitu wazazi, kama unataka kumfanya mwanao wa kike mtaji basi mtaji mkubwa ni kumpa elimu na si kumuozesha, mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume,” anasema.

Mara kadhaa Naibu Katibu Mkuu wizara ya elimu Dk Avemaria Semakafu amekuwa akizungumzia namna ambavyo watoto wa kike wakipata elimu wanavyoweza kuwa msaada mkubwa.

“Ukimkomboa mwanamke kielimu ni sawa na kuikomboa jamii nzima, ndio sababu natamani kuona wanawake wengi wakijitosa kwenye masomo ya sayansi. Sio kweli kwamba masomo haya ni magumu kiasi cha kuwashinda watoto wa kike; kinachotakiwa ni utayari wa mwanafunzi husika kujifunza. Tunahitaji kuwa na wanawake wengi katika fani za sayansi,” alisema Dk Semakafu wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri mwaka 2019 katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).