Aliyekuwa katibu mkuu Chadema aacha utata

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa ameongozana na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji (kushoto) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita wakati wa kesi za viongozi wa chama hicho. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ameibua utata kufuatia maandishi yake aliyoweka katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana kuzua mjadala.

Huo ulikuwa mwendelezo wa kauli tata za Dk Mashinji tangu Chadema ichague na kuteua safu yake mpya ya uongozi huku wadhifa wa Katibu Mkuu aliokuwa akiushikilia akipewa John Mnyika.

Gazeti hili jana lilimkariri Dk Mashinji akimwonya Mnyika atekeleze majukumu yake kwa ufanisi na aepushe chama hicho kuhodhiwa na watu wachache.

Dk Mashinji alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tangu mwaka 2016.

Chadema wiki hii ilifanya uchaguzi wake na kupata viongozi mbalimbali.

Mbali na uteuzi wa Mnyika, ambaye ni mbunge wa Kibamba, Chadema ilimrejesha Freeman Mbowe katika nafasi ya uenyekiti.

Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara huku Issa Said Mohamed akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa Zanzibar.

Nafasi ya Mnyika ya Naibu Katibu Mkuu (Bara) ilijazwa na Singo Benson Kigaila na Salum Mwalimu akibaki kama Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, viongozi wa kuteuliwa hutakiwa kukaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano, kabla ya kuongezewa muda au kuachwa.

Awali, Dk Mashinji aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akimpongeza Mbowe kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Chadema kwa kipindi cha miaka mingine mitano.

“Pia, nimpongeze Mh. T. Lissu na Mh. Issa Said Mohammed, nyote kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema. Mungu awatangulie nyote katika kutekeleza majukumu yenu!”

Baada ya hapo aliandika ujumbe mwingine ambao ndiyo umezua utata miongoni mwa wasomaji wake, akisema;

“Haikuwa rahisi lakini tumetoka wote salama na tukiwa wamoja. Kichwani mwa kila kiongozi kumejaa siri nyingi sana... Eeh, Mungu mwenye enzi, nakushukuru sana kwa kutulinda mpaka tukatoka salama. Asanteni wana Chadema wote, na Watanzania kwa ushirikiano mwema!”

Baadhi ya wachangiaji katika ujumbe huo walikuwa na maoni tofauti akiwemo Gwamaka Alipipi (Gwamaka Alipipi @AlipipiG, akihoji; “Unamshukuru Mungu kwa kutoka salama?????”

Mwingine (Angry Citizen) alihoji “Kichwani kwa kila kiongozi kumejaa siri nyingi sanaa??”

Clever Son Of Africa @AfricaClever, alimshauri Mashinji, “Vincent hii ni Noeli nikuombe sana ubaki ndani ya nyumba yetu, naamini bado tunakuhitaji sana. Najua kuna watu wanakutamani kwa ajili ya kutugawa.”

Naye Mr Ndikwegha @ndikwega alimpongeza Dk Mashinji, “Hongera sana tunaendelea kukutambua kama mtu muhimu sana kwenye chama chetu cha Chadema na kama alivyosema mwenyekiti kwenye chama kuna kazi nyingi sana zinahitaji watu wenye uwezo mkubwa, imani yangu ni kwamba bado upo na kazi kubwa ya chama.”

Hata hivyo, Chiggs @Chiggs47931521 alisema, “Aina ya watu kama Dr Mashinji na siasa za Chadema ni `incompatible’ (vitu tofauti) kabisa. `Professionalism and diligence aren’t something to be embraced at all by Chadema’s’. (Weledi na bidii ni vitu visivyotiliwa maanani na watu wote Chadema). Kutoka salama ni neno kubwa sana unaweza andikia kitabu ukiwa mchambuzi wa mambo ya kisiasa.”

Mchangiaji mweingine mr Bulinjiye @BulinjiyeF alisema, “Maneno hayo yanajenga taharuki kwa watu wanaofikiria vyema. Kukaa kimya nako ni kuzuri zaidi kuliko kuibua mijadala yenye faida kwa wengine kaka.”

Mbali na sintofahamu hiyo kwenye mtandao wa Twitter, Dk Mashinji alikaririwa na Mwananchi jana akimpongeza mrithi wake Mnyika, huku akimtaka kusimamia majukumu yake ili chama hicho kisihodhiwe na watu fulani ingawa hakufafanua.

“Mnyika nimekuwa naye, nampongeza sana, anaelewa vizuri nilikuwa nasimamia nini katika utekelezaji wa majukumu yangu.Ahakikishe anasimamia vyema majukumu yake ili Chadema iwe taasisi imara na siyo mali ya watu fulani,” alisema Dk Mashinji.

Alipotafutwa kwa simu ili kupata ufafanuzi wa kauli zake, Dk Mashinji hakupokea.

Wachambuzi wanasemaje?

Baadhi ya wasomi waliozungumza na Mwananchi wamemshauri kutulia ili kulinda masilahi ya chama hicho.

Mwanasheria Dk Onesmo Kyauke alisema hata kama Dk Mashinji hakuridhishwa na hatua hiyo anapaswa kulinda masilahi ya chama chake.

“Unajua kwenye siasa ni sawa na ilivyo kwenye kampuni, inafika mahali muda wako unaisha. Kwa mwanasiasa mzuri huwezi ukazungumza mambo ya kampuni yako.

“Hata walivyo CCM si unaona wanabadilisha makatibu wakuu kulingana na mahitaji yao? Kwa sababu katibu ndiyo mtendaji mkuu wa chama, kama wameona wampe mtu mwingine, yeye angetulia tu,” alisema Dk Kyauke.

Aliongeza, “Hata kama ana malalamiko yake, kwa mtu imara au muungwana huwezi ukaenda kutangaza huko nje. Hata kama ingekuwa ni kampuni, kwa mfano wewe ulikuwa meneja wa benki wasipoendeleza mkataba wako, huwezi kwenda kutangaza siri ya biashara ya benki hiyo.”

Akizungumzia utendaji wa Dk Mashinji, Dk Kyauke alisema hakuweza kuvaa viatu vya Dk Wilbrod Slaa.

“Kwa kweli baada ya Dk Slaa kuondoka pale Chadema, chama kilitetereka kidogo pamoja na kwamba kilifanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Unajua katibu anatakiwa kuwa mtu anayezifahamu siasa na akiongea awe anasikilizwa,” alisema.

Aliendelea, “Kwa bahati mbaya, Dk Mashinji hakuwa `politician’ (mwanasiasa) na ndiyo maana alikua hajulikani, yaani alikuwa akiongea mahali fulani hawatilii maanani tofauti na alivyokuwa Dk Slaa kwenye nafasi ya Katibu Mkuu.”

Mhadhiri wa shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa alimtaka Dk Mashinji kuchagua moja; kueleza waziwazi kinachomsibu au kukaa kimya ili kulinda masilahi ya chama chake.

“Kama kuna kutoridhika, wanasiasa wanahitaji kuwa wajasiri na yeye wakati anateuliwa, aliyemteua alisema ni mtu jasiri na aliweza hata kuongoza madaktari walipokuwa wakidai masilahi yao.

“Kwa hiyo ujasiri pengine inabidi awe nao kama kuna jambo analo ni vizuri basi akawaeleza Watanzania,” alisema Dk Kahangwa.

Aliongeza, “Lakini akiona hakuna haja basi anyamaze ili kukilinda chama chake. Kama anataka kusema azungumze waziwazi kuliko kuweka mafumbo ambayo yatawafanya watu watunge mambo yao.”