Asasi zadai wabakaji wa ‘teleza’ wameibuka tena, polisi yakanusha

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno

Dar es Salaam. Umoja wa asasi za kiraia umemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani kufanya ziara wilayani Kigoma kushuhudia matukio ya wanaume wanaojipaka mafuta kuepuka kukamatwa baada ya kubaka wanawake nyakati za usiku.

Matukio kama hayo yaliwahi kuibuka katika Kata ya Mwanga Kusini mwaka 2016 na wakati huo polisi ilisema ilimkamata kijana mmoja kwa tuhuma za kuvamia nyumba za wanawake na kuwabaka.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alisema kuwa hajawahi kusikia uwapo wa watu hao wala matukio ya aina hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga alisema kuwa matukio hayo yaliwahi kutokea mwaka 2016 na yaliisha.

Lakini mratibu wa miradi wa shirika la Tamasha, Annagrace Rwehumbiza aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wakati wakifanya shughuli za ulagibishi mkoani Kigoma walitaarifiwa kuwa bado yanafanyika.

“Nilizunguka mitaa miwili kwa siku mbili na kupata kesi za watu 45 waliobakwa na teleza,” alisema Rwehumbiza.

Jina la “teleza” limetokana na watu hao kujipaka mafuta machafu hivyo inakuwa vigumu kuwakamata kwa kuwa wanateleza.

Miongoni mwa asasi zilizoshiriki kuweka hadharani simulizi za wanawake waliovamiwa na kubakwa ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tamasha, Change Tanzania, Kituo cha Madai Mkakati, Jamii Forums na Twaweza.

Asasi hizo zimedai kuwa wanaofanyiwa vitendo hivyo wanatoa taarifa kwa mamlaka husika na hawaoni hatua zikichukuliwa, hivyo kuiomba wizara hiyo kufanya ziara maeneo hayo ili kushuhudia.

‘Nilijeruhiwa kwa panga’

Wakizungumza katika mkutano huo na waandishi, baadhi ya walioathirika walisema wabakaji hao hutumia silaha pia.

Mmoja wa wanawake hao, Ramla Issa alisema mvamizi alibomoa matofali matatu chini ya dirisha la nyumba yake na kuingia.

Alisema baada ya kupiga kelele alijeruhiwa na panga mikononi kwa sababu alikuwa anakinga asipigwe usoni.

Alisema alipokwenda kutoa taarifa kwa mamlaka husika, alijikuta akipachikwa jina la “mke wa teleza”.

Mbali ya simulizi hiyo, meneja utetezi wa Twaweza, Anastazia Rugaba alisema msichana wa miaka 36 alidai kuwa aliingiliwa na ‘teleza’ mara sita na kujeruhiwa mara nne kwa nyakati tofauti, mara ya mwisho ikiwa mwaka huu.

Alisema tukio jingine ni la kubakwa mama mwenye mimba ya miezi nane mbele ya watoto.

Pia alisema mwanamke wa miaka 60 aliwahi kupigwa nondo baada ya kupiga kelele.

“Wapo hadi wazee wa miaka 70 mtu na dada yake wameingiliwa na teleza mara mbili kila mmoja,” alisema Rugaba, huku akionyesha video za kinamama hao wakizungumza.

Naye Churchill Shakim, mkurugenzi mtendaji wa Tamasha, alisema bado kunahitajika hatua zaidi kukomesha vitendo hivyo.

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema jukumu la kukemea tabia hizo ni la jamii nzima.