Askofu awakemea wanaume tegemezi

Dodoma. Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecoste Bible Fellowship Tanzania (PBFCT), Jafeth Mapogo amekemea tabia ya baadhi ya wanaume wasiofanya kazi badala yake, wanawaachia majukumu yote wake zao.

Alitoa kauli hiyo juzi akihubiri kwenye makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Dodoma Makulu jijini hapa.

Alisema kumekuwa na tabia ya wanaume maarufu marioo, kutofanya kazi na kuwaachia majukumu yote ya familia wake zao kwani haifai katika jamii.

“Mwanaume akishaoa anashinda amekaa nyumbani hafanyi kazi ya aina yoyote, anamwacha mama wa watu ahudumie familia yeye amekaa tu bila kazi yoyote hii tabia ife,” alisema Askofu Mapogo.

Askofu Mapogo alisema dhana ya hapa kazi tu imeanzia kwenye vitabu vyote vya dini katika Biblia Mtume Paulo aliwaambia Wakristo kuwa asiyefanya kazi na asile na kuwataka waumini wa kanisa hilo kutowapa chakula wavivu.

Alisema tabia ya uvivu miongoni mwa watu ndiyo inayosababisha kufa kwa kukosa maarifa kwa kudhani kuwa baraka zinapatikana bila kufanya kazi. “Mungu hawezi kukubariki bila kufanya kazi… hata Ibrahim ambaye tunamjua ni baba wa imani alikuwa anafanya kazi alikuwa analima na kufuga ndiyo maana Mungu alimbariki sasa nyie hata kazi hamtaki kufanya halafu mnataka baraka?” alihoji.

Muumini mmoja wa kanisa hilo, Joshua Peter alisema mahubiri hayo yamekuwa somo kwa vijana kwani hawataoa mpaka wawe na kazi nzuri za kutunza familia zao.

Naye Frank Sonyo alisema mahubiri hayo yamekuja wakati mwafaka kwa sababu wanawake wakijishughulisha na kazi mbalimbali huku wanaume wakikaa vijiweni