Baraza laitwa kumng’oa meya, korti ikitupa maombi yake

Meye wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (kushoto) akizungumza na wakili wake Barnabasi Nyalusi baada ya kusikiliza hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi wa Iringa, Aden Kanje iliyotupilia mbali maombi yake ya kuzuia mchakato wa Baraza la Madiwani kumuondoa madarakani jana. Picha na Said Ng’amilo.

Iringa. Saa chache baada ya Mahakama ya Mkoa kutupa maombi ya kuzuia mchakato kumng’oa meya ya Manspaa ya Iringa, Alex Kimbe, Baraza Maalumu la Madiwani limeitisha kikao kinachoaminika kitahitimisha suala hilo.

Kikao hicho kilichoitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, kitafanyika leo saa 4:00 asubuhi katika ukumbi wa Manispaa ili kukamilisha majukumu ya mkutano ulioahirishwa Machi 26.

Taarifa ya mkutano huo kwa wananchi iliyosainiwa na ofisa habari wa manispaa, Siima Bingileki inasema kikao hicho kimeitishwa chini ya kanuni ya 9(4) ya kanuni za kudumu za manispaa zilizotolewa mwaka 2015.

Mapema jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Iringa iliyotoa maamuzi ya mapingamizi ya serikali dhidi ya maombi ya Meya Kimbe ikisema alikosea katika kuyawasilisha.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Aden Kanje alisema kutokana na kukosea vifungu, mahakama imeona maombi hayo hayana mashiko

Mahakama hiyo ilipokea maombi ya meya kuzuia mchakato wa kung’olewa Machi 12, 2020 na upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi Machi 17 na kusikilizwa siku hiyo hiyo.

Hakimu Kanje alisema amesikiliza hoja za pande zote zilizojikita katika mamlaka ya mahakama ya kuzuia mchakato wa kumng’oa meya, na kubaini kuwa “mamlaka ya mahakama yana mipaka kisheria na huwa ni ya mpito ya siku 90 na si ya kudumu, kama alivyokuwa anaomba meya”.

Akizungumza nje ya mahakama, wakili wa meya huyo, Barnabas Nyalusi alisema anasubiri nakala ya uamuzi huo ili ashauriane na mteja wake kuhusu hatua ya kufuata.

“Hakimu hajafuta kesi bali amesema vifungu ambavyo tumetumia katika maombi yetu havikuwa sahihi, kwa hiyo lazima tukasome tena vifungu na kushauriana na mteja wangu,” alisema.

Alisema mteja wake alikuwa anazuia mchakato wa kumtoa meya madarakani, hakuzuia meya kuondolewa kwa kuamini mchakato huo haukufuata sheria.

“Kanuni za kudumu za manispaa zinaeleza wazi ili meya aondolewe ni vitu gani vinatakiwa vifuatwe,” alisema.