VIDEO: Bashiru: Mchakato wa katiba ni kiporo kilichochacha, hakiliki

Dar es Salaam. Wakati mjadala ukiendelea kuibuka upya, katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amefananisha kukwama kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya na kiporo cha chakula ambacho “kimechacha na hakiwezi kulika tena”.

Lakini, mtendaji huyo mkuu wa chama tawala ameendelea na msimamo wake wa kutaka mjadala huo uendelee na watu waachwe wazungumzie masuala ya nchi yao kwa kuwa mwishoni yatasaidia kupatikana kwa Katiba mpya itakayojibu mahitaji kwa wakati husika.

Amesema hayo wakati wanasiasa, wanaharakati na taasisi mbalimbali zikizungumzia haja ya kuandika Katiba mpya kwa kumalizia mchakato uliokwama mwaka 2015 katika hatua ya kupiga kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, huku takriban theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la Katiba ikiwa imesusia vikao katika hatua ya mwanzo ya kujadili Rasimu ya Katiba.

Dk Bashiru alisema hayo jana katika mahojiano na Mwananchi alipotembelea makao makuu ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti pamoja na MCL Digital.

Alisema hayo wakati akijibu swali kuhusu kutofautiana kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na msimamo wa CCM kuhusu ujamaa. Kwamba Katiba inataja ujamaa tofauti na chama.

Katika mahojiano hayo yaliyorushwa moja kwa moja na MCL Digital na ambayo yalichukua takriban saa tatu (2.53), Dk Bashiru alizungumzia jinsi nchi za Kiafrika zilivyoanzisha itikadi yake kutokana na historia ya kutawaliwa na hivyo katiba ni lazima zizingatie utu, haki, uhuru.

Dk Bashiru alisema mijadala kuhusu Katiba inapaswa kuendelea ili kupata muafaka wa masuala yanayopaswa kuridhiwa na wananchi ili yawekwe katika nyaraka hiyo muhimu kulingana na mazingira ya sasa.

“Mimi msimamo wangu utabaki palepale, hautabadilika na pia ndio msimamo wa chama changu (CCM); waachwe wananchi wazungumze kuhusu masuala ya nchi yao. Mjadala ni kitu muhimu sana,” alisema Dk Bashiru.

Alisema msingi wa itikadi za siasa za Afrika ni ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kifikra kwa sababu bara hili ndilo pekee duniani ambalo “watu wake waliuzwa sokoni kama kuku” kwa miaka 400 kwa nia ya kupata malighafi, soko, na nguvukazi ya bure na baadaye kwenda kuzitajirisha nchi zao.

“Leo sasa itikadi itakayotufaa ni vijana kubaki Afrika kujenga uchumi wa kiafrika, kuwa na fikra za kimaendeleo kiafrika, kuwa na soko la maendeleo la Afrika, na kuzalisha malighafi kwa viwanda vya kiafrika,” alisema Dk Bashiru.

“Kwa hiyo kwangu mimi, tungeingia katika mjadala wa Katiba, tungeafikiana ni itikadi gani tuitangaze katika Katiba yetu ambayo kila chama kitakachoingia madarakani, kisimamie ukombozi wetu. Kwamba asitokee mtu akashawishika akasema ‘hapana bwana, bora nikawe mbwa wa Ulaya kuliko kuwa raia wa Tanzania.”

Alisema kutokana na misingi hiyo ya ujamaa inayojali utu, haki usawa na uhuru, haoni kama wananchi wanaweza kubishania mambo hayo katika mjadala wa Katiba.

“Tunaweza kubishana katika mkakati wa kufikia huko; kwamba mbona mnasema utu lakini utu wa watu unadhalilishwa? Mbona mnasema haki, wakati haki haitendwi? Mbona mnasema usawa wakati hakuna mgawanyo sawa? Na tukawa tunashindana kwa wananchi ni chama gani kinaweza-- kwa kweli-- kusimamia misingi hiyo ya utu, haki, usawa na uhuru,” alisema.

“Bahati mbaya hatukuweza kumaliza kiporo. Na kiporo hicho hakiwezi kulika tena. Kimechacha. Tutapata matatizo ya tumbo na kiafya. Kwa kweli sidhani kama kinafaa tena.

“Ni kiporo. Sasa nani alisababisha kuwe na kiporo? Tunaanza kunyoosheana vidole na nisingependa tufikishane huko. Mahali pa kuanzia ni kutambua kwamba tulisukumana kwenda kupata Katiba mpya hatukufika na kuna makosa yamefanyika. Sasa tutafakari kuyasahihisha ili tupike chakula kipya, safi na cha lishe.

“Wakati tukifanya hivyo, Katiba hizi tulizonazo tuziheshimu na mamlaka zilizopo kikatiba zitende haki ili mchakato uanze upya na mzuri zaidi uwepo. Ni lini? Mimi sijui kwa sababu sikujua kama nitakuwa katiba mkuu.”

Licha ya mchakato huo kukwama kutokana na Tume ya Uchaguzi (NEC) kutokamilisha usajili wa wapigakura, ulishaingia dosari mapema wakati wa kujadili muundo wa Muungano baada ya baadhi ya wajumbe kudai CCM ilipeleka rasimu tofauti na ile iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, wakidai ndiyo iliyotoka kwa wananchi.

Mjadala huo umekuwa ukiibuka taratibu kutokana na watu tofauti kueleza haja ya kuandika Katiba mpya.

Februari 10, Jaji Warioba alisema anaamini kuwapo kwa matamanio ya wananchi juu ya kutimizwa jambo hilo kwa kutumia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni ili kuuhitimisha mchakato huo.

“Tumeanza mwaka 2013, mimi ninaamini kazi kubwa imeshafanyika ya kufikia Katiba mpya.” alisema Jaji Warioba alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Alichokisema Jaji Warioba kinafanana na kile kilichosemwa mwezi mmoja uliopita na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) kwamba litaanza midahalo ya kudai Katiba mpya.

Thamani ya CCM Sh1 trilioni

Katika mahojiano ya jana, Dk Bashiru aliulizwa swali linalohusu ukimya wa utekelezaji wa mapendekezo ya kamati aliyoiongoza kufanya uhakiki wa mali za chama hicho nchi nzima, ambapo alieleza utekelezaji unafanyika.

Dk Bashiru aliyeanza kuongoza taasisi hiyo Mei 29 mwaka juzi akichukua nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyestaafu, alisema kamati aliyoiongoza ilitakiwa ipendekeze namna ya kuzuia wizi wa mali za chama.

“Siku tunamkabidhi mwenyekiti (Rais John Magufuli) alionya kuwa humo kwenye ripoti tukianza kufukua kaburi tutakosa mahali pa kuyaweka lakini tunataka ripoti hii ituzuie kuendelea na ufujaji wa mali za chama,” alisema Dk Bashiru.

“Nilipoingia walikuwa wanasema thamani ya mali za chama ni Sh50 bilioni. Tumefanya tathimini tumepata inafikia Sh1 trilioni,” alisema.