Bashiru awashukia wenye ajenda ya tume huru 2020

Dodoma. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali amesema wanaodai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ni viongozi wanaotaka kufika Ikulu “ndani ya wiki moja”.

Dk Bashiru amesema, wanaodai tume huru ya uchaguzi wanapaswa kutambua kuwa suala hilo si la muda mfupi bali ni mchakato unaopaswa kupitia hatua tofauti.

Alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Kauli ya Dk Bashiru, ambaye ni mtendaji mkuu wa CCM, imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la kudai tume huru ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Vuguvugu hilo lilishika kasi baada ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kususiwa na vyama vya upinzani kwa maelezo kuwa wasimamizi walikuwa wakiwafanyia vitendo vya kuwazuia kushiriki, wagombea kukamatwa na mawakala kuzuiwa. Maeneo mengi wagombea wa CCM walipita bila ya kupingwa na hivyo kutokuwapo na upigaji kura na chama hicho kikashinda kwa zaidi ya asilimia 90.

Kwa sasa vyama vya siasa, baadhi ya wa wasomi na wanaharakati wanaona kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi ndio kutapunguza malalamiko katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jijini Dar es Salaam hivi karibuni kwamba chama chake kimemwandikia barua Rais John Magufuli kuhusu umuhimu wa kutungwa sheria itakayowezesha kuwapo tume huru kabla ya uchaguzi wa Oktoba.

Hata hivyo, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Serikali au Chadema wenyewe kuhusu majibu ya ombi hilo. Hata hivyo, Magufuli akizungumza katika hafla na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, alisema uchgauzi mkuu utakuwa huru na haki na kwamba utaendeshwa katika misingi ya uwazi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wakuu wa Chadema, ambacho ni chama kikuu cha upinzani, walirejea wito wa kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Walisema hayo wakati wakitoa salaam za pole kwenye msiba wa Elias Mwingira (baba wa Mtume Josephat Mwingira wa kanisa la Efata), Kibaha mkoani Pwani. Kadhalika viongozi hao walimwomba Mtume Mwingira azungumze na viongozi wenzake wa madhehebu ya dini kuliombea taifa na uchaguzi mkuu wa 2020 ili haki itamalaki kwa kupatikana tume huru.

Juzi baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, walionekana kuunga mkono matakwa ya kuwapo kwa tume huru, japokuwa walitofautiana katika mtazamo wa jinsi ya utekelezaji. Wakati wakiunga mkono suala hilo, wapo waliosema kinachopaswa kutangulia ni Katiba mpya ambayo uwepo wake utakidhi matakwa ya tume inayodaiwa na masuala mengine muhimu ya kidemokrasia.

Kauli ya Dk Bashiru

Jana Dk Bashiru naye alizungumzia suala la Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, akisema wanaohimiza suala hilo wana ajenda ya kuwahi Ikulu.

Alikuwa akijibu swali kuhusu video fupi inayozunguka kwenye mitandao ikimhusisha na dai la katiba mpya, kauli ambayo alikiri jana kuwa ni ya kwake. Video hiyo ilirekodiwa katika moja ya mijadala wakati wa mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya mwaka 2014, Dk Bashiru alisema “hakuna anayebisha kuwa yapo mahitaji makubwa ya kuwa na katiba mpya kwa sababu ndiyo medani ya kujenga muafaka katika mfumo wa vyama vingi”.

Jana, katibu huyo alisema wanasiasa wamekuwa na kelele za kudai tume huru na katiba mpya wakitaka mambo yaende kwa haraka, lakini hawajui kila jambo linapaswa kuwa na utaratibu wake.

“Ukisikiliza wanasiasa watakwambia tunataka tume huru, kesho watasema tunataka katiba mpya. Mimi nakubali suala la katiba mpya kuwa ni ajenda ya wananchi, lakini inapokuja kuwa ajenda ya wanasiasa ndiyo tunapata shida,” alisema Dk Bashiru.

Alisema baadhi ya wanasiasa ambao wanaitafuta Ikulu ndani ya wiki moja, ndiyo wamekuwa wakipiga kelele kuhusu tume huru na katiba lakini akasema siku zote mambo mazuri hayawezi kufanywa kwa haraka kiasi hicho.

Kuhusu Katiba, alisema hata kama itachelewa na kuja wakati watu wameshakuwa wazee, bado kuna vizazi ambavyo vitanufaika nayo, hivyo ni ajenda ambayo anaikubali.

Alisema kelele za wanasiasa waliodai Katiba, ndizo zilisababisha kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini walipokosa kuingia Ikulu umoja huo, hauna kichwa, miguu, mikono wala macho.

Kadhalika alizungumzia kauli yake alipokuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu Watanzania kutaka katiba, akasema kauli yake ni ndiyo msimamo wake ingawa anaamini kuwa ni ajenda ya wananchi na wakati ukifika wataamua.

“Ni kauli yangu ile, nilizungumza kwa dakika 45 lakini nashangaa kinazunguka kipande kidogo tu cha dakika mbili au tatu, wangesikiliza mahojiano yote wangeona nilizungumzia nini, narudia kuwa, katiba mpya ni ajenda ya wananchi haiwezi kufa kwa sababu za wanasiasa,” alisema Dk Bashiru.

Katika hatua nyingine Dk Bashiru alizungumzia kuhama kwa wanasiasa akisema kata na majimbo wanayowakilisha yako kwenye mikono salama ya serikali ya CCM.