Bosco Ntaganda, mbabe wa kivita anayekwenda kusubiri uzee akiwa jela

Saturday November 9 2019

 

Nguvu za kijeshi na ulinzi mkali uliomzunguka kila mara havikuweza kumsaidia mbabe wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Bosco Ntaganda kuepuka kifungo jela.

Ntaganda (46) aliyepewa jina la ‘Terminator’, likimaanisha alikuwa ndiye mmaliziaji wa maisha, juzi Alhamisi alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu (ICC).

Hukumu hiyo ambayo ndiyo ya juu kuwa kutolewa na mahakama hiyo iliyopo The Hague, Uholanzi, ilisomwa na Jaji Robert Flemr baada ya kumkuta na hatia ya mashtaka 18 dhidi yake likiwamo la kusimamia watu kuuawa kwa kuchinjwa, kupondwa vichwa na kunyofolewa viungo vya ndani.

Ntaganda alitiwa hatiani mwezi Julai kwa uhalifu huo yakiwamo mauaji, unyanyasaji na kufanya utumwa wa kingoni na mauaji mengi ya halaiki ya raia wa DRC katika eneo la Ituri lenye madini mengi kati ya mwaka 2002 na 2003.

Wanajeshi watiifu kwake waliendesha mauaji ya kuchinja watu wengi katika mashamba ya migomba nyuma ya kijiji ambao watu 49 wakiwamo watoto na vichanga walinyofolewa viungo vya ndani au vichwa vyao kupondwapondwa.

Ntaganda pia alikuwa anawajibika kwa mashtaka ya ubakaji na kuteka mabinti wadogo kwa ajili ya ngono na kusajili jeshini watoto chini ya miaka 15.

Advertisement

Baada ya kufafanua mashtaka hayo aliyotiwa hatiani, Jaji Flemr alimweleza Ntaganda kuwa “kifungo chako kwa ujumla kitakuwa ni miaka 30 jela.

Ikiwa atamaliza muda huo, bila kuhesabu punguzo ambalo huwa linatolewa, mbabe huyo wa kivita atatoka gerezani akiwa na umri wa miaka 76.

Majaji wa kesi hiyo walimhukumu kifungo cha juu kinachotolewa na ICC kwa maana ya idadi ya miaka, lakini walisema makosa yake hayakidhi kifungo cha muda wote.

Ntaganda, akiwa katika suti na shati la bluu na tai nyekundu, aliketi bila kujitingisha katika mahakama iliyojaa ulinzi wa nguvu, wakati akisikiliza hukumu dhidi yake kupitia vinasa sauti vya masikioni.

Msemaji wa ICC amesema hiyo ndiyo adhabu kubwa kuwahi kutolewa na mahakama hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2002 kwa ajili ya makosa makubwa duniani.

Majaji wamesema Ntaganda alikuwa kiongozi katili wa kikundi cha Kitutsi, kilichoendesha vita vilivyoivuruga DRC baada ya mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda.

Wameongeza kuwa Ntaganda alikuwa kiongozi muhimu wa kikundi cha waasi cha Union of Congolese Patriots na tawi lake la kijeshi – Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC).

Sehemu kubwa ya mashtaka dhidi yake yalihusu mauaji yaliyofanywa na wanajeshi watiifu kwake dhidi ya raia vijijini mwaka 2002 na 2003.

Mahakama ilisikiliza ushahidi wanavijiji waliojawa na hofu wakimwita Ntaganda “Terminator”, wakimfananisha na filamu ya Arnold Schwarzenegger iliyojaa mauaji ya kikatili yaliyokuwa yanafanywa na roboti.

Kwa ujumla, Ntaganda alipatikana na hatia kwa makosa 13 ya uhalifu wa kivita na mengine matano ya uhalifu dhidi ya binadamu na kuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa na ICC kwa kosa la kuteka wasichana kwa ajili ya ngono.

Vilevile alikuwa mtuhumiwa wa kwanza kujisalimisha kwa ICC, akijipeleka katika Ubalozi wa Marekani uliopo Kigali nchini Rwanda mwaka 2013 na kuomba apelekwe mahakamani nchini Uholanzi.

Mwezi Septemba, majaji wa ICC, waliwasikiliza tena kwa nyakati tofauti waathirika na mashahidi, ikiwa ni miezi miwili baada ya kumtia hatiani Ntaganda, ili waweze kuamua adhabu.

Zaidi ya watu 60,000 waliuawa tangu mashambulizi hayo yalipoanza katika Mkoa wa Ituri mwaka 1999, kwa mujibu wa taasisi za haki za binadamu, wakati vikundi vya wanamgambo vikishambuliana ili kumiliki eneo lenye rasilimali za madini.

Ntaganda aliwaeleza majaji wakati wa usikilizaji wa kesi dhidi yake kuwa alikuwa askari na si mhalifu na kuwa jina la utani la Terminator halikuwa lake.

Baada ya mgogoro wa Ituri, Ntaganda aliingizwa katika Jeshi la Congo na aliteuliwa kuwa jenerali kuanzia mwaka 2007 hadi 2012, lakini baadaye akawa mwanzilishi wa kikundi cha waasi cha M23 na vuguvugu jipya dhidi ya serikali.

Waendesha mashtaka walisema uamuzi wake wa kujisalimisha ICC wakati huo ulilenga kujilinda mwenyewe kwa alikuwa hatarini kutokana na uhasama uliokuwapo kati ya vikosi vya waasi.

Huyo ni mmoja wa wababe watano wa kivita kutoka Congo kuwahi kushtakiwa katika ICC tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

Bosi wake wa zamani, Kamanda wa FPLC Thomas Lubanga alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela mwaka 2002.

Lakini kwa siku za karibuni ICC imekuwa ikilaumiwa kwa washtakiwa wengi wakubwa wanaofikishwa hapo kuachiwa huru, akiwamo kiongozi wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo aliyeachiwa mapema mwaka huu.

Imelaumiwa pia kwamba zaidi imekuwa ikisikiliza tu mashauri ya viongozi wa Waafrika.

Advertisement