Bunge labadili uendeshaji TLS, viongozi wasema hawajui

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi akiwasilisha bungeni muswada wa sheria ya marekebiusho ya sheria mbalimbali (Na.8) wa mwaka 2019, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Bunge limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019 ambao ndani yake una sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), iliyofanyiwa marekebisho yaliyotajwa na baadhi ya wabunge kuwa yanakibana chama hicho.

Juzi katika mjadala wa muswada huo, wabunge wa upinzani walipinga baadhi ya mabadiliko huku wale wa CCM wakimuunga mkono Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alipokuwa akijibu hoja za wapinzani.

Baada ya Bunge kupitisha muswada, jana Mwananchi ilizungumza na rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala, ambaye alisema hawajapata nakala za mabadiliko hayo.

“Tulitoa maoni na mapendekezo yetu mbele ya kamati ya Bunge, tuliamini wenzetu wametuelewa,” alieleza Nshala.

Alipoulizwa ikitokea marekebisho hayo yatakinzana na mapendekezo yao, Dk Nshala alisema, “baada ya kuiona sheria, baraza la uongozi (la TLS) litakaa kujadili na kuona hatua zaidi za kuchukua”.

Katika mabadiliko hayo, hoja zilizotikisa mjadala wa Bunge ni mkutano mkuu wa TLS kuwa na uwakilishi wa kikanda tofauti na awali ambapo wanasheria wote walishiriki.

Sasa zitaundwa kanda maalumu za mawakili ambao watatengeneza muundo wa kuwapata wawakilishi wao kwenye mkutano huo.

Hata hivyo, pendekezo la TLS kutaka rais wa chama hicho kukaa madarakani miaka mitatu badala ya mmoja, lilikataliwa.

Mbali na TLS, mabadiliko mengine yaliyokuwepo katika muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ni kuhusu sheria ya uvuvi ambapo wabunge waliona adhabu iliyopendekezwa na Serikali ni kubwa.

Licha ya hoja za wapinzani zilizoongozwa na mbunge wa viti maalum (Chadema), Salome Makamba kuibuliwa, muswada huo ulipitishwa na Bunge.

Kubadili mfumo wa TLS kulipingwa na mawakili wakati wa vikao vya kamati ya Bunge, waliolalamika kuwa wataminywa uhuru wao.

Kabla ya kuwasilishwa bungeni, Dk Nshala alikaririwa akisema kuwa muswada huo kama ungepitishwa jinsi ulivyo, nguvu ya mawakili ingepungua na itakuwa gharama kwao kwani wawakilishi wa kanda watatakiwa kulipiwa gharama za mkutano wakati kwa sasa wajumbe wanajilipia wenyewe.

Walichokisema wabunge

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisimamia hoja hiyo akitaka sheria ya mawakili ibaki kama ilivyo sasa kwa kuwa inajitosheleza lakini Profesa Kilangi alisema jambo hilo ni gumu.

“Mnataka kuwaminya mawakili, Serikali inatumia mabavu kupora haki za watu, mbona hawa wanajitegemea wenyewe kwa kila kitu kwa nini tuwapunguze kwenye mikutano yao, hili si jambo jema hata kidogo,” alisema Msigwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema siyo busara hata kidogo kuwaingilia wanasheria katika mikutano yao kama ambavyo Serikali inataka kwani hoja ya wingi siyo tatizo kwa kuwa ziko nchi zenye mawakili wengi lakini wanakutana hivyo itakuwa jambo geni kwa Tanzania kuwa na mkutano wa uwakilishi.

Peneza alitolea mfano wa nchi ya Kenya kwamba ina mawakili zaidi ya 9,000 wakati Nigeria wapo milioni 1.5 lakini wanakutana kwa pamoja akahoji iweje Tanzania waambiwe kuwa wapo wengi na kudai Serikali inatengeneza mazingira ya kuiua taasisi hiyo.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Saleh alisema, “mnataka kuiua TLS na kuifanya chombo cha serikali, niseme tu muda ndio unazungumza maana leo mnasema ni wanaharakati hivi hamjui kuwa miongoni mwao anaweza kuchaguliwa Rais anayetokana na CCM, kama mnasema hivyo ina maana mnazuia uanaharakati ambao ni haki ya kila mtu?”

Mbunge wa Mbinga mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema muundo wa TLS ulivyo kwa sasa haufai ni lazima ubadilishwe kwa kuwa umepitwa na wakati.

Mapunda alisema sheria hiyo ilitungwa mwaka 1954 ambapo Taifa lilikuwa na mawakili 14 waliokuwa na uwezo wa kukaa chumba kimoja na kujadiliana jambo kwa pamoja.

“Haiwezekani, kumbuka hata kwenye kamati walikuja wenyewe wakatuambia kuwa pamoja na kuwa wanakaribia 8000 kwa idadi yao, lakini kwenye mkutano mkuu Arusha hawajawahi kufika hata 2000, hii inaonyesha wanahitaji uwakilishi,” alisema Mapunda.

Makamba na Dk Kilangi

Bunge lilipokaa kama kamati Dk Kilangi alichuana vikali na Makamba kuhusu maeneo hayo mawili.

Makamba alikuwa akisisitiza TLS kuingiliwa na kupokonywa uhuru wao na akataka jambo hilo liachwe kwani linakwenda kuitia doa serikali.

Akijibu hoja hizo, Profesa Kilangi alisema sheria ya mawakili ilitungwa na Bunge hivyo hakuna ubaya kama chombo hicho kimeamua kuifanyia marekebisho kwani kisheria mawakili nao ni sehemu ya serikali na hivyo hawawezi kuachwa wakajiendesha wenyewe.

Kilangi alisema TLS siyo taasisi binafsi kama inavyotafsiriwa, kwa kuwa hata kuanzishwa kwake ilipitishwa kwa sheria ya Bunge hivyo inapaswa kuangaliwa na kurekebishwa ndani ya chombo hicho.

Sheria ya Uvuvi

Wabunge wa CCM, Dk Charles Tizeba na Joseph Mkundi wao walisimamia kupinga adhabu kwa watu wanatajwa kuwa ni wavuvi haramu kwamba adhabu ya Sh2 milioni hadi Sh10 milioni ni kubwa kwa wananchi wa kipato cha aina ya wavuvi kwani wengi wataozea gerezani ilivyopendekezwa kwenye mabadiliko ya sheria ya uvuvi.