Butiku atamani watu 467 waliokiri uhujumu uchumi watajwe majina

Thursday October 10 2019

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku 

By Noor Shija, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mchakato wa msamaha kwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi wanaokiri makosa na kulipa fedha zilizo katika mashtaka yao unashika kasi, lakini mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku anadhani ungeboreshwa zaidi.

Anatamani watuhumiwa 467 ambao Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alitangaza kuwa wamekiri makosa na wako tayari kulipa fedha, watajwe majina yao na watu waliokuwa wakishirikiana nao.

“Rais (John) Magufuli anasema kama tungeachana na rushwa nchi yetu ingeendelea,” alisema Butiku katika mahojiano maalumu na Mwananchi wiki iliyopita.

“Matokeo ya rushwa ni hawa 467, walikuwa wanashirikiana na nani ndani na nje? Kwanini walifanya hivyo na sheria zipo?”

Butiku alikuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere tangu akiwa madarakani hadi alipofariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyopo London nchini Uingereza na mahojiano hayo ni mfululizo wa makala ambazo Mwananchi inazifanya kuelekea Oktoba 14, siku ambayo Mwalimu Nyerere alifariki miaka 20 iliyopita.

Alikuwa akizungumzia mpango wa Rais Magufuli wa kutangaza msamaha wa siku 14, akitaka wote wenye makosa ya kuhujumu uchumi wakiri makosa yao na wawe tayari kulipa fedha kwa kiwango kilichopo kwenye mashtaka yao na hivyo kutoka jela. Kosa la uhujumu uchumi halina dhamana.

Advertisement

Takribani wiki moja baada ya muda wa awali aliotoa rais kuisha, DPP Mganga alieleza kuwa watu 467 wamejitokeza kukiri na wako tayari kulipa Sh107 bilioni na akaomba ziongezwe siku tatu kuwapa nafasi wengi zaidi kujitokeza, na Magufuli akampa siku saba.

“Unaweza kuwa na watu 467 waliokuwa wamekusanya fedha za umma. Watu 467 Sh107 bilioni, (hawa) wangeorodheshwa majina,” alisema.

“Bahati mbaya hapa tunaficha, ingekuwa ile nchi za wenzetu wangewaorodhesha majina. Hivi ni akina nani hawa na walikuwa wanashirikiana na nani?

“Hivyo, kabla ya kurekebisha haya, fedha zilikuwa zinapotea, zilikuwa zinakwenda kwenye mifuko ya nani. Hili jambo ni kubwa sana. Rais amelitangaza, lakini watu wanaliona kama jambo dogo.”

Butiku alisema waliochukua fedha hizo ni Watanzania walioamua kunyang’anya hata wajukuu zao.

“Nataka tulijadili kwa kina kwa sababu Rais ameanzisha utaratibu wa pekee wa kuambizana kweli, halafu tuelewane, halafu tusameheane,” alisema Butiku.

“Halafu tuseme nyinyi mliofanya msirudie na nyinyi mliokuwa mnafanya hamkujulikana msirudie na sisi ambao tulikuwa hatujafanya kamwe tusirudie kusudi tupate amani ya kweli.

“Na watu wa nje tuwaambie hivi msitushawishi kuingia katika mambo ya rushwa na mtutendee haki katika kuwekeza hapa. Muwekeze mpate chenu cha haki na sisi tupate cha haki.

“Msiwe na mfumo wa kutudanganya na kutuibia na katika mfumo wa biashara tutendeane haki (ili) mazao yetu yapate bei stahili na vitu vyenu mtuuzie kwa bei stahili ili utu wetu na haki yetu ikamilike.”

Kauli hiyo ya Butiku aliyekuwa anazungumzia uadilifu wa enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere enzi za uongozi wake, alisema katika miaka 20 bila Mwalimu mambo ya msingi ya kukumbuka ni haki ya msingi katika utu.

“Wote tupate mahitaji ya msingi, wote tupate chakula cha kushiba, wote tuwe na nyumba nzuri ambazo tunaweza tukapata usingizi. Wote tutembee tukiwa na uhakika wa usalama wa maisha yetu kwamba hakuna mtu anayeweza kutoka akatupiga mkuki,” alisema Butiku.

Alisema haki ya msingi iliyosisitizwa na Mwalimu ni pamoja na watoto wapate elimu bora, iwe kwenye shule binafsi au shule za serikali.

“Sasa hivi elimu na mnajua kuna ubaguzi kidogo. Ukijenga shule ya binafsi inakuwa kama nongwa, lakini unachangia kufundisha watoto,” alisema.

Butiku alisema misingi ya haki aliyoisisitiza Mwalimu inataka watu wote wamiliki ardhi ya kulima na kupata bei nzuri ya mazao wanayozalisha.

Biashara na mataifa mengine

Kuhusu ushiriki wa Tanzania kimataifa katika masuala ya biashara, Butiku alisema nchi imekuwa ikiibiwa kwa kupangiwa bei ndogo ya mazao inayouza, lakini bidhaa kutoka nje zinaingia kwa gharama kubwa.

“Pamba tunauza kwa bei ndogo na pia dhahabu, lakini vitu tunavyonunua kutoka kwa wenzetu waliochukua malighafi kwetu, tunanunua kwa bei kubwa,” alisema.

“Anayetupangia bei ya pamba ndiye anatupangia bei ya magari.”

Alisema Mwalimu aliwahi kusema huo ndio mfumo unaotuibia na kusababisha madeni makubwa kwa Taifa.

“Sasa inapokuja kwenye uchumi, hasa uwiano wa biashara, unapata nini katika vile unavyouza na unauza kwa bei gani, ile tofauti ndiyo inafanya unapata madeni unalazimika kukopa. Jasho lako (lakini) hupati pato la kukutosha,” alisema.

“Mwalimu amekufa anasema tukiendelea na mfumo huo tunauza rahisi tunanunua ghali, ndani yake tunaibiwa na tumeibiwa sana (lakini) tunaridhika tu.

“Mwalimu ametoka anauliza mfumo huo mnataka tuubadili kwa mazungumzo au tena kwa vita kama tulivyopigana wakati wa ukoloni.”

Alisema kinachofanywa na Rais John Magufuli kulinda rasilimali za nchi ndicho kilichokuwa kimedhamiriwa na Mwalimu Nyerere katika kujenga misingi ya haki na utu.

“Utu na usawa wake na haki ya uchumi, haki ya siasa tumeipigania tunasema tunajitawala, lakini kweli tunajitawala vizuri? Tuna nguvu gani tunaweza kulinda mipaka yetu?” alihoji Butiku.

Hoja ya Mwalimu kisiasa

Kuhusu mabadiliko ya kisiasa, Butiku alisema anadhani aliyoyataka Nyerere yapo.

“Ukisikiliza sasa hivi katika mfumo wa vyama utasikia wachache wanasema uhuru wetu haujakamilika, haki yetu haijakamilika. Wengi nao wanasema hivyo ubishi huo ni wa kawaida,” alisema.

Butiku pia alizungumzia uamuzi wa Serikali kuruhusu siasa za vyama vingi mwaka 1992 baada ya Tume ya Jaji Francis Nyalali kuzunguka nchi nzima kutafuta maoni ya wananchi na matokeo kuonyesha asilimia 20 tu ndio waliotaka mabadiliko hayo.

Alisema wale asilimia 80 waliokataa mfumo wa chama kimoja walikuwa na sharti lenye mambo 10 waliyotaka yatekelezwe.

“Mwalimu akasema nyinyi chama changu (CCM), hawa wanaotaka chama kimoja wana haya mambo 10, Mkibaki pekee yenu mnayaweza? Akasema ‘kwa maoni yangu hamtayaweza na upinzani mkubwa ni katika haya 10,” alisema Butiku.

“Kwa hiyo tukubali tukae nyumba moja. Tusaidiane kubishana lakini tuko katika nyumba moja. Mzee (Ali Hassan. Rais wa Awamu ya Pili) Mwinyi akasema tukikaa nyumba moja tutawekeana utaratibu wa kuzungumza ili tuzungumze kwa kusikilizana tusizungumze kwa makelele wengine wanatupa mawe wakiwa nje.

“Msingi wa vyama vingi ndiyo huo. Mnatofautiana mawazo lakini mnaendelea kuheshimiana na mnazungumza kwa utaratibu ili mpate muafaka kama si leo basi kesho.”

Nafasi ya pekee

Alisema kitendo cha Mwalimu kukemea pale Serikali inapokwenda kinyume kilitokana na yeye Nyerere kuwa Baba wa Taifa, hivyo alikuwa na nafasi ya pekee ya kukemea wadogo zake.

“Msingi wake ulikuwa ni ule. Mwalimu hakuogopa wala hakuwa na aibu. Aliheshimu katika misingi kwamba nina heshimu utu wako, anapoona unatetereka kwa kuacha misingi inayojenga amani na utulivu anakuambia palepale, usiposikia atakukemea,” alisema Butiku.

Alisema kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliikemea Marekani kutokana na tabia yake ya kuziminya nchi ndogo.

“Tanzania tulileta mambo yetu 68, yajadiliwe, yapitishwe na yakubaliwe katika hayo ni manne tu ambayo Marekani ilikubali, mengine yote mkapiga kura ya veto mkafanya kampeni yasipite,” alisema akimkariri Mwalimu wakati akihutubia Umoja wa Mataifa.

Butiku alisema Mwalimu alipomaliza kuhutubia msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, alimfuata kumuuliza kwamba alikuwa na ulazima gani kutoa maneno yale.

“Mwalimu alimjibu kuwa alipaswa kuyasema, pia alifafanua kuwa Marekani ni taifa kubwa kijeshi, kiuchumi, kisiasa na lenye sauti kubwa, lakini halisikilizi ‘ilibidi niwakemee na nitaendelea kufanya hivyo,” alimnukuu Mwalimu.

Butiku alisema tabia ya Mwalimu ya kukemea ni ngumu kuigwa kama mtu hana imani na watu.

Kujenga Taifa

Butiku alisema Mwalimu kwenye hotuba yake ya kuapishwa kuwa Rais mwaka 1962, alisema kujenga taifa si kujenga barabara, majumba, kujenga shule au vyuo vikuu.

Alisema kujenga taifa kwa maneno ya Mwalimu ni kujenga tabia ya watu wenye maadili yanayowawezesha kuishi kama wamoja, wakiheshimiana, wakisaidiana, wakitendeana haki ili wawe taifa la amani, umoja na maendeleo.

“Mwalimu siku zote alisema utu wa kila mtu utambuliwe na uheshimiwe, haki za kila mtu atendewe na apewe na pale ambapo hazipo,” alisema.

Advertisement