Bweni shule ya Kiislam lateketea kwa moto

Muktasari:

Vitu mbalimbali vya wanafunzi vimeteketea moto



Moshi. Wanafunzi zaidi ya 50 wa Shule ya Sekondari Uchira Islamic iliyo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamenusurika kuungua baada ya bweni la kuteketea kwa moto.

Hii ni shule ya tisa katika mfululizo wa shule zilizopo chini ya taasisi za Kiislamu kuungua tangu matukio hayo yaanze kujitokeza yakianzia Jijini Dar es Salaam na baadhi ya maeneo kusababisha vifo.

Mkuu wa shule hiyo ya Uchira Islamic, Abdukahari Mfinanga alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wanafunzi walipokuwa nje ya bweni hilo.

“Hili bweni linatumiwa na wanafunzi wa kike zaidi ya 50 tunatumia umeme wa jua (solar) lakini tunashangaa moto ulipotokea hapajulikani,” alisema mkuu huyo wa shule.

“Vitu mbalimbali vya wanafunzi vimeteketea moto yakiwamo magodoro na mabegi, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh15 milioni. Chanzo cha moto hatujakijua lakini tunahisi ni hujuma.”

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shabani Mlewa alisema bado hawajakutana kujadili tukio hilo na sasa suala hilo linashughulikiwa na makao makuu ya Bakwata.

“Serikali inaendelea na uchunguzi sababu tatizo limekuwa kubwa wanafuatilia kwa kina na wao watatuambia; wametuomba tufanye subira. Ila wiki ijayo tumeitisha kikao cha masheikh,” alisema Sheikh Mlewa.

“Hadi sasa kuna shule tisa za Kiislam sehemu mbalimbali nchini zimeshaungua moto; kwa hiyo nawaomba tufanye subira kwa ajili ya kusubiri wakati jambo likiwa kwenye upelelezi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Emanuel Lukula alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokewa.