CAG afichua matatizo kwenye sekta ya maji

Dodoma/Moshi. Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini matatizo mengi kwenye sekta ya maji yakiwamo ya hasara kubwa inayosababishwa na upotevu wa maji, kutotekelezwa kwa miradi na uchimbaji wa visima unaotoa maji yenye mushkeli.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ambaye aliwasilisha ripoti yake bungeni Jumatatu iliyopita, alisema matatizo hayo ni kipimo cha utendaji na ufanisi mdogo kwenye sekta ya maji.

CAG anasema licha ya umuhimu wa maji katika maisha ya binadamu na maendeleo, usambazaji wa maji nchini umekuwa hafifu na hausambazwi kwa wakati na ubora.

Upotevu wa maji

Kichere alisema upotevu huo wa maji uliosababisha hasara ya Sh155.84 bilioni unatokana na uvujaji wa maji, msukumo wa maji na uunganishaji haramu.

Alieleza mkataba kati ya Wizara ya Maji na mamlaka za maji unaelekeza kiwango cha maji kinachopotea kisizidi asilimia 20.

Alisema ukaguzi wake uliofanyika katika mamlaka 20 za maji kuhusu upotevu wa maji, uligundua mamlaka moja tu ya Kahama ndiyo ilikuwa na asilimia inayovumilika kwenye upotevu wa maji.

“Mamlaka 19 zilizobaki ziliendelea kupata hasara inayotokana na upotevu wa maji kwa kiasi zaidi ya kiwango cha uhimilivu cha upotevu wa maji.

“Kiasi cha upotevu kwa mamlaka zote hizi kilikuwa Sh155.84 bilioni ambacho ni zaidi ya kiwango cha uhimilivu wa upotevu ambacho ni Sh74.14 bilioni.

“Hii inamaanisha kwamba tofauti ya Sh 81.70 bilioni ilikuwa katika kiwango kisichohimilika cha upotevu kulingana na taarifa zilizopo za kiwango cha maji kinachozalishwa na idadi ya wateja waliounganishwa,” alisema.

Alisema anapendekeza mamlaka za maji mijini zipunguze kiwango pendekezwa kilichowekwa cha upotevu wa maji kwa kusimika mita kwa wateja wote, kuhimili msukumo wa maji kwenye eneo la usambazaji, pamoja na kubadilisha mifumo chakavu na kuweka miundombinu na vifaa vipya.

Pia, alisema amebaini kuwa mikoa 13 ikiwamo ya Dar es Salaam na Dodoma, imetajwa kutoa huduma ya maji chini ya saa 24, tofauti na inavyotakiwa.

Kichere ilibainisha kuwa mikoa hiyo inakwenda kinyume na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji inayotaka mamlaka ya maji kutoa huduma kwa wastani wa saa 24 kila siku.

Aliitaja mikoa hiyo inayotoa huduma chini ya saa 24 ni Morogoro (saa 12), Lindi (saa 14), Arusha na Kigoma (saa 15), Singida, Dar es Salaam (saa 21), Mwanza (saa 22), Dodoma na Tanga (saa 23).

Pia, wilaya za Musoma (Mara), Masasi na Nachingwea (Lindi), Bukoba (Kagera) zinatoa kwa saa 22, Babati (Manyara) saa 17 na Chalinze (Pwani) saa 18.

Usambazaji maji upo chini ya malengo

Pia CAG amebaini kuwa kwa miaka mitano, Wizara ya Maji ya Tanzania imeshindwa kufikia lengo lake la kusambaza maji vijijini kwa asilimia 76.5.

Katika ripoti yake jumla ya ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalum wa CAG uliofanywa katika kipindi kilichoishia Machi 31, 2020, CAG amebainisha kuporomoka kwa usambazaji maji kwa wananchi vijijini.

Kuhusu malengo ya wizara kutofikiwa kwa miaka mitano, CAG amebainisha kuwa mapitio ya ripoti ya utendaji kazi wa Wizara hiyo wa mwaka 2018, yanaonesha hadi 2017/2018 walifikia asilimia 58.7.

Mapitio ya ripoti ya utendaji kazi ya Wizara ya Maji ilionyesha hadi kufikia mwaka wa fedha 2017/18 asilimia 58.7 tu ya watu wanaoishi vijijini ndiyo wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama. “Kwa kipindi cha miaka mitano Wizara ya Maji imeshindwa kufikia malengo yake ya kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa waishio vijijini unakuwa asilimia 76.5 hadi kufikia mwaka 2015,” imesema ripoti hiyo.

CAG alisema mwaka 2015/2016 kiwango cha juu cha upatikanaji wa maji kilikuwa asilimia 74 lakini kikashuka hadi asilimia 58.7, na hiyo ni kwa mujibu wa halmashauri 12 zilizotembelewa.

“Hii inaonyesha kuwa upatikanaji maji safi na salama vijijini umepungua kwa asilimia 13.88 ikilinganishwa na mwaka 2016/17,” anasema CAG katika ripoti hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake.

CAG anasema uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama unatokana na mapungufu wakati wa maandalizi ya Miradi ya Maji iliyopelekea miundombinu ya maji kujengwa bila kuwa na vyanzo vyenye uhakika.

Katika ripoti yake hiyo, CAG anasema licha ya kuwapo kwa bajeti ya kutosha, bado Wizara ya Maji haikuhakikisha kuwapo kwa rasilimali za kutosha kwa ajili ya kutoa huduma ya majisafi na maji taka.

“Ilibainika kuwa Mamlaka za Serikali za Mtaa na Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira hazina mikakati endelevu ya kutenga bajeti kwa ajili ya miradi ya maji,” anasema katika taarifa hiyo.

Matokeo yake, CAG anasema kumekuwapo na kutokukamilika kwa miradi ya maji iliyoanzishwa na kumekuwepo ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha kuwapo kwa riba.