CAG avianika CCM Chadema, CUF

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ameibua kasoro katika hesabu za vyama vitatu vya siasa vya Chadema, CCM na CUF.

Ripoti hiyo ya mwaka unayoishia Juni 30, 2019 iliyowasilishwa bungeni Dodoma jana imefafanua kile alichodokeza CAG Charles Kichere alipowasilisha ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli kuhusu CUF kuwa ilipokea Sh422.9 milioni kwenye moja ya akaunti zake za benki, fedha ambazo chanzo chake hakikuthibitishwa.

“Pia, nilibaini kuwa kati ya magari 16 yanayomilikiwa na CUF, saba yalionekana kuwa na usajili wa jina la CUF, wakati mengine tisa yalisajiliwa kwa majina ya wanachama wa CUF.

“Kadhalika, nilibaini kuwapo mkopo wa Sh85 milioni uliotolewa na CUF kwa moja ya kituo cha redio huko Tanga ambao haujarejeshwa,” imesema ripoti hiyo.

Katika ripoti hiyo, CAG pia alibaini kuwepo kwa kituo cha redio kilichotajwa kilikuwa na wakurugenzi watatu, ambao pia ni viongozi wa CUF. “Kupitia ukaguzi wangu, nilibaini kuwa CUF ilihamisha Sh300 milioni kwenda kwenye akaunti binafsi ya mmoja wa wanachama wa CUF na kiasi cha Sh60 milioni kilitolewa taslimu,” imesema ripoti hiyo na kuongeza;

“Hata hivyo, hakuna kumbukumbu za matumizi zilizowasilishwa kwa ajili ya ukaguzi. Pamoja na hayo, Sh47 milioni zilitolewa kama fedha taslimu kutoka katika akaunti ya Benki ya CUF na mmoja wa wakurugenzi wa chama hicho bila idhini ya katibu mkuu.Katika mapendekezo yake, CAG ameitaka CUF kuboresha mifumo yake ili kupunguza hatari za udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za wanachama.

“Kadhalika, uchunguzi unapaswa kuanzishwa ili kupata ukweli wa matumizi ya Sh416 milioni yaliyotolewa kimashaka kwenye akaunti za benki za CUF,” imesema ripoti hiyo. Mbali na CUF, ripoti hiyo pia imefichua kuwa CCM inamiliki viwanja 5,660 Tanzania Bara na Zanzibar, lakini kati ya hivyo, viwanja 5,261 havina hatimiliki.

“Pia, nilibaini Jumuiya ya Wazazi (CCM) ilimfukuza mpangaji iliyempangisha kwenye moja ya vyumba vyake kwa njia isiyokuwa halali; na ililipa Sh60 milioni kama fidia ya kumwondoa mpangaji huyo bila ya kufuata taratibu,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

CAG pia amebaini kuwa Shirika la Uchumi na Kilimo la Dar es salaam (Sukidar) la CCM lilisaini makubaliano na kampuni ya Korea ya kuanzisha kampuni ya huduma ya tiba. “Hata hivyo, niligundua kuwa hakuna mkurugenzi kutoka CCM aliyeteuliwa kwenye bodi ya wakurugenzi ya kampuni iliyoundwa tofauti na masharti ya makubaliano,” imesema ripoti.

Kwa upande wa Chadema, ripoti hiyo imebaini kuwepo matumizi ya Sh205.41 milioni bila ya idhini ya halmashauri kuu ya chama hicho.

Mbali na vyama hivyo, CAG pia alibaini Sh2.13 bilioni zilitumiwa na vyama vya siasa 11 bila ya kuwa na nyaraka tosholezi. Pia, CAG aligundua vyama vya siasa vinne havikuandaa rejista ya wanachama. Mbali na hayo, nilibaini vyama vya siasa vinane kati ya 19 vilivyokaguliwa havikuandaa taarifa za usuluhushi wa kibenki wa kila mwezi.

“Kwa kuongezea, nilibaini vyama vya DP, CCK, na CHAUMMA havikuwasilisha mali zinazomiliki kwa Msajili wa vyama vya siasa,” imesema ripoti.

Pia mapitio ya CAG yalionyesha Sh534.84 milioni zilikusanywa na vyama vya siasa tisa.

“Hata hivyo, kiasi kilichopokelewa hakikuwasilishwa kwenye akaunti za benki za vyama husika. Kwa kuongezea, nilibaini vyama vya siasa tisa vimetayarisha taarifa zao za kifedha bila kutamka mfumo uliotumika kuandaa taarifa za fedha,” imesema ripoti hiyo.