CCM yajigamba ushindi wa kisulisuli Jimbo la Lema Arusha

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitapata ushindi wa kisulisuli Mkoani Arusha katika uchaguzi wa serikali za Mitaa.

Arusha. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema wanatarajia kupata ushindi wa kisulisuli katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumapili Novemba 17, 2019 Jijini hapa akiwa ameambatana na makatibu waenezi wa chama hicho kutoka wilaya za Mkoa wa Arusha, amesema hakuna shaka yoyote ushindi watakaoupata.

“Tuliambiwa hapa Arusha Mjini ni ngome ya mbunge fulani wa chama cha bwana Mbowe, Arusha wakati wote imekua ya CCM na sasa namwambia mbunge wa hapa atafute kazi nyingine mwaka 2020, nimesikia eti anaenda kugombea Kilimanjaro huko asijisumbue tumeshamaliza kazi,” amesema Polepole.

Kuhusu Wilaya ya Ngorongoro, amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya elimu kwa kuwa na shule za msingi na Sekondari za bweni kuwawezesha wanafunzi wa jamii ya wafugaji kupata elimu bila usumbufu.