CCM yamng’oa M’kiti wa wilaya

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Dodoma Mjini Robert Muwinje akizungumza kwenye moja ya vikao vya chama hicho. Picha na Maktaba

Muktasari:

Mwenyewe asema amepokea barua ambayo haielewi inalenga nini kwa madai kuwa kilichoandikwa hakiendani na uhalisia

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Dodoma Mjini, Robert Muwinje amevuliwa wadhifa wake.

Hata hivyo, viongozi wa CCM wamekuwa na kigugumizi cha kueleza mkasa kuhusu kiongozi huyo licha ya taarifa kueleza kuwa alikuwa na makosa ya kiutumishi ambayo yeye (Muwinje) amesema hayajui.

Taarifa kutoka ndani ya ofisi ya wilaya, zinaeleza kuwa Muwinje aliondolewa Desemba 2019 baada ya kikao cha halmashauri kuu ya Taifa ya CCM kilichokutana jijini Mwanza.

Katika kikao hicho, CCM ilipendekeza kuwaita kwenye kamati ya maadili makatibu wakuu wastaafu Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba pamoja na kada maarufu wa chama hicho Benard Membe.

Alipoulizwa iwapo amepokea barua ya kuondolewa katika nafasi yake, Muwinje alikiri kuipokea huku akisema bado anatafakari kwa kuwa anakipenda chama chake.

“Siwezi kusema nimefukuzwa au kama nipo ofisini, lakini nina barua ambayo huenda siielewi vizuri inalenga nini maana kilichoandikwa hakiendani na uhalisia na inatoka ngazi za juu ila ikiwa hivyo nitaheshimu uamuzi wa chama,” alisema Muwinje bila kueleza ni ngazi ipi ilimuandikia barua.

Kada huyo ambaye alitumikia nafasi ya mwenyekiti wa vijana Wilaya ya Dodoma Mjini na kumaliza salama, alianza kukumbwa na misukosuko kutoka kwa makada wenzake huku baadhi wakimtuhumu kuwa upendo wake kwa wanachama unaweza kuwa mwiba katika nafasi za kisiasa atakazoendelea kugombea.

Mmoja wa wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu mikoa ya kanda ya ziwa, alikiri jina la Muwinje kupelekwa katika kikao hicho na uamuzi kutolewa baada ya kujiridhisha kuwa alikuwa na tuhuma zinazohusu matumizi mabaya ya ofisi.

Kada huyo alisema wamemuandikia mashtaka 19 na kisha kumpeleka ofisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili akachunguzwe na baadhi ya tuhuma ziko chini ya uongozi wa chama.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alipoulizwa kuhusu tuhuma za Muwinje hakuwa tayari kuzungumza huku akisisitiza wafuatwe viongozi wa CCM.

Marafiki wa karibu wa mwenyekiti huyo kutoka ndani ya chama, wametaja moja ya sababu ya kuondolewa ilitokana na misimamo ya kiongozi huyo wakati wa kuchuja majina ya walioomba nafasi za wenyeviti wa mitaa kwa jiji la Dodoma kwa kupitisha jina la mgombea aliyekuwa amekataliwa na vikao vya chini.

Katibu wa CCM wa Mkoa, Jamila Yusufu alikataa kulizungumzia jambo hilo akisema liko juu ya uwezo wake, hivyo akashauri watafutwe viongozi wa ngazi za juu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, hakukubali wala kukataa kuhusu kuondolewa kwa mwenyekiti huyo badala yake aliomba watafutwe viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Katibu Mkuu Dk Bashiru Ali au Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole.

“Jambo hilo ni zito kijana wangu, lakini kama unataka kujua kama lipo au halipo wapigie wasemaji wa chama ambao ni katibu mkuu, ukimkosa mpigie katibu wa itikadi na uenezi watakuwa na majibu,” alisema Mkanwa.

Akizungumza kwa njia ya simu, katibu mkuu Dk Bashiru Ali alimtaka mwandishi kuwasiliana na katibu wa itikadi na uenezi Humphrey Polepole ili azungumzie hilo.

Alipotafutwa Polepole, alihoji kuhusu taarifa hizo akitaka waulizwe ngazi ya mkoa wazungumze.

Hata hivyo, baada ya kuelezwa kuwa mkoa umerusha mpira kwake akasema, “nimekusikia naomba unipe muda kidogo halafu nitakurudia ili kukuambia kuna nini Dodoma.”

Baada ya hapo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi hakujibu ingawa taarifa zimesambaa wilaya nzima kuhusu kuondolewa kwa kada huyo.