Chadema, ACT Wazalendo kuja na mkakati mwingine

Muktasari:

Baada ya mpango wa kufanya maandamano yasiyo na kikomo nchini nzima kushinikiza kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu kukwama, huku viongozi kadhaa wakikamatwa, vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimesema vinajipanga kuja na mkakati mwingine.

Dar/Mikoani. Baada ya mpango wa kufanya maandamano yasiyo na kikomo nchini nzima kushinikiza kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu kukwama, huku viongozi kadhaa wakikamatwa, vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimesema vinajipanga kuja na mkakati mwingine.

Hayo yalielezwa jana na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe baada ya kuripoti kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wawili hao wakiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika Oktoba 31 walitangaza maandamano yasiyo na kikomo na walipanga yaanze Novemba 2.

Hata hivyo, kabla ya siku hiyo kufika, polisi walimkamata Mbowe, wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema, Godlbess Lema na Boniface Jacob na siku tatu baadaye Zitto ambaye alikwenda kituoni kuwajulia hali wenzake, huku mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee akijisalimisha siku hiyo.

Lakini Novemba 2, viongozi hao waliachiwa na kutakiwa kuripoti polisi jana, siku ambayo wametakiwa kuripoti tena kituoni hapo Jumatatu ijayo.

Mbali na viongozi hao, Lissu naye alikamatwa akiwa nje ya ofisi za Umoja wa Ulaya (EU) lakini aliachiwa muda mfupi baadaye.

Wakati wao wakiachiwa, hadi jana saa 10:00 jioni wanachama 18 wa vyama hivyo walikuwa wakishikiliwa polisi baada ya kukamatwa kuanzia Oktoba 28.

Katika maelezo yake jana, Zitto alisema vyama vyote vinaendelea na vikao ili kujua nini cha kufanya na kuendelea kujipanga dhidi ya madai yao.

“Vikao vya vyama vinaendelea kujua nini cha kufanya ili kujipanga zaidi, lakini maandamano yetu yasiyokuwa na kikomo yako palepale,” alisema Zitto.

Wanaoshikiliwa polisi

Watu 18 kutoka mikoa tofauti wameendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu siku ya uchaguzi mkuu.

Miongoni mwao, 11 wapo mkoani Arusha na ambao jalada lao limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, mmoja kutoka Katavi na saba kutoka mkoani Mbeya.

Wakati huohuo, wafuasi 10 kutoka vyama tofauti waliokuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam wameachiwa kwa dhamana.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa watuhumia hao, Kamanda wa polisi wa Arusha, Salum Hamduni alisema tayari uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao 11 umekamilika na watafikishwa mahakamani.

Wakati kamanda Hamduni akisema hayo mwishoni mwa wiki, katibu wa Chadema wa mkoa alisema wanachama zaidi ya 34 walikuwa wamekamatwa kutokana ma vurugu za uchaguzi.

Wakati watuhumiwa hao wakisubiri kufikishwa mahakamani, mkoani Mbeya makada saba wa vyama vya siasa kati ya 13 bado wanaendelea kushikiliwa Jeshi la Polisi kwa mahojiano kutokana na makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushawishi maandamano, vurugu na kujeruhi watu siku ya kupiga kura.

Akizungumza na Mwananchi, kamanda wa polisi wa mkoa, Ulrich Matei alisema wengine wameachiwa kwa dhamana lakini kwa waliobakia (7) uchunguzi unaendelea na watafikishwa mahakamani.

Alisema kabla ya siku ya kupiga kura, baadhi ya wafuasi na makada wa vyama vya siasa, waliungana na kushawishi wanachama wao kufanya maandamano katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Mbeya

“Siku ya kwanza walifika wakaimba lakini sisi tulikaa kimya. Walipochoka waliondoka na kurejea siku ya pili wakiwa wameandamana pia, jambo ambalo kama polisi tulilazimika kuchukua hatua za kisheria dhidi yao kwa kusababisha shughuli kukwama kutokana na kelele nje la lango kuu,” alisema.

Aidha, Kamanda Matei aliwatahadharisha makada wa vyama vya siasa kutumia busara katika kipindi hiki na wasiwatumie wananchi kama chambo kwa kuwashawishi kuandamana, kufanya vurugu kwa kujua Serikali imelala.

Jijini Dar es Salaam, kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema wafuasi 10 waliokuwa wameendelea kushikiliwa na jeshi hilo baada ya wengine kuachiwa, nao wameachiwa.

Mkoani Katavi, Ng’wailwa James anaendelea kushikiliwa kwa kuwarushia mawe askari polisi wawili waliokuwa wakilinda amani baada ya uchaguzi.

Kamanda wa polisi mkoa huo, Benjamini Kuzaga alisema Oktoba 29 saa 2:30 usiku askari polisi wakiwa katika doria ya kulinda amani na kutuliza ghasia zinazoweza kujitokeza baada ya uchaguzi, walikutana na kikundi cha watu wachache waliokuwa wanataka kuvuruga amani.

“Baada ya kutakiwa kutawanyika waliokuwa waelewa walitekeleza lakini baadhi walikaidi, tulitumia nguvu ya kadri kuweza kuwatawanyisha, kabla hatujawatawanyisha huyu mtuhumiwa akiwa na wenzake kwenye hilo kundi tunaoendelea kuwatafuta pia, aliwarushia mawe askari wakiwa kwenye gari la polisi na wenzake na kusababisha askari wawili kujeruhiwa’’, alisema.”

Imeandikwa na Fortune Francis, Mary Clemence, Mussa Juma, Hawa Mathias na Aurea Simtowe