Chadema mpya itaweka historia uchaguzi mkuu mwakani?

Mwenyekiti  wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa amebebwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho baada ya kuchaguliwa juzi usiku jijini Dar es Salaam  Picha na Ericky Boniphace

Katika uchaguzi mkuu wa 2015, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka historia kwa kufanya vizuri katika kinyang’anyiro cha urais kwa kuibuka na kura nyingi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Wakati huo Chadema ilimsimamisha Edward Lowassa chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na Chadema yenyewe, CUF, NCCR Mageuzi na NLD.

Lowassa alisimamishwa kuwania urais na umoja huo baada ya kujiunga na Chadema akitokea CCM ambako jina lake lilikatwa katika mbio za kuwania kuteuliwa na chama kuwania nafasi ya urais.

Hata hivyo, ujio wa Lowassa ulisababisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa kujiuzulu nafasi hiyo na kutimkia ng’ambo akitangaza kuacha siasa.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa Chadema alipata kura zaidi ya milioni sita, huku mshindi kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli akipata kura zaidi ya milioni nane.

Miaka minne imepita na sasa Chadema kimepanga upya safu yake ya uongozi ambayo itadumu madarakani kwa miaka mitano ijayo.

Viongozi waliochaguliwa ni Freeman Mbowe (mwenyekiti) ambaye ametetea nafasi hiyo, Tundu Lissu (makamu mwenyekiti-Bara) n Issa Mohamed Issa (makamu mwenyekiti-Zanzibar).

Viongozi wengine walioteuliwa ni Katibu Mkuu, John Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, Benson Kigaila (naibu katibu mkuu-Bara) na Salum Mwalim (naibu katibu mkuu-Zanzibar).

Wakati viongozi hao wakichaguliwa kuongoza Chadema, mazingira ya kufanya siasa yamebadilika tofauti na miaka minne iliyopita. Je mikakati waliyonayo viongozi hao itaiwezesha Chadema kufanya vema katika uchaguzi mkuu ujao?

Wataweza kuvunja rekodi waliyoiweka katika uchaguzi mkuu wa 2015? Au yaliyotokea yataendelea kubaki kuwa historia?

Inafahamika baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015, Rais Magufuli alipiga marufuku kufanyika mikutano ya hadhara na maandamano hadi 2020 na kutaka viongozi waliochaguliwa ndio wafanye mikutano hiyo kwenye maeneo yao.

Agizo hilo limekuwa mwiba kwa viongozi wa vyama vya upinzani ambao mara kadhaa wamejikuta katika wakati mgumu na kukamatwa hata pale wanapofanya mikutano ya ndani.

Wakati agizo hilo likitekelezwa, madai ya msingi ya vyama vya upinzani ni kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi ambayo wameidai kwa muda mrefu sasa.

Pamoja na kilio hicho, hivi karibuni mwenyekiti wa Chadema aliomba kuwapo kwa maridhiano ya kitaifa ili kuwapo uwanja sawa wa kufanya siasa.

Madai hayo na mengine kuhusu uchaguzi bado hayajafanyiwa kazi. Kutotekelezwa kwa madai hayo kunakifanya chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuwa njia panda kuelekea 2020. Je kitaweza kutimiza ndoto zake za kushika dola katika mazingira kama haya?

Katibu Mkuu

Katibu Mkuu mpya wa Chadema, John Mnyika anasema kazi yake ya kwanza yeye na wenzake katika sekretarieti ya chama ni kuongoza Chadema kuchukua dola mwaka 2020.

Anasema katika kutekeleza kazi hiyo wana vipaumbele vitano ambavyo ni kudai tume huru ya uchaguzi kwa njia mbalimbali, kuandaa wagombea na kufanya maandalizi ya ilani ya uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Anasema vipaumbele vingine ni kuendeleza kazi ya Chadema ni msingi, ili kuwa na mtandao thabiti wa chama pamoja na kuendeleza Chadema Digital.

“Tunahitaji nguvu ya umma kwa upande mmoja na nguvu ya Mungu kwa upande mwingine, ili mabadiliko katika taifa letu yaweze kutimia,” anasema Mnyika.

Alipoulizwa iwapo madai ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi hayatafanikiwa kabla ya uchaguzi mkuu mwakani chama kifanyaje, Mnyika anasema kuwa chama hicho kitashinda kwa kutumia nguvu umma.

“Ndio maana tumesema tunaanza maandalizi mapema ya kuwapata wagombea wetu kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2020. Tuna mikakati mingi ya kufanya ili kuhakikisha tunashinda.

“Huu mfumo wa Chadema ni msingi unatuwezesha kuwa na mtaji mkubwa wa wanachama,” anasema.

Mnyika anasema kuwa kupitia Chadema Digital watakuwa na mfumo wa ukusanyaji matokeo katika kila kituo na hivyo kujihakikishia ushindi.

“Isipopatikana tume huru ya uchaguzi, tuna njia nyingi za ziada za kuzitumia ila kwa sasa siwezi kuzitaja kwa kuwa tunaweza kumpa mbinu adui yetu,” anasema.

Anasema kuwa mfumo watakaoutumia ni wa kisasa zaidi tofauti na ule walioutumia mwaka 2015 ambao ulikuwa rahisi kudhibitiwa.

“Wakati ule tulikuwa tunatumia taasisi mbili kukusanya matokeo. Tutakaotumia 2020 ni mfumo tofauti hawataweza kudhibiti upokeaji matokeo yetu. Tutatumia teknolojia ya kisasa sana,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu alisema sasa chama kina nguvu kuliko ilivyokuwa awali na kwamba wanafanya maandalizi ya kutosha katika muda uliobaki kuelekea 2020, ili wairudishe nchi katika demokrasia ya kweli.

“Baada ya yote tuliyofanyiwa njia iliyobaki ni kuchukua nchi mwaka ujao. Leo tuna nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa juzi na jana. Tufanye maandalizi ya kutosha, ili ngwe iliyobaki tuweze kuirudisha nchi katika misingi yake ya haki,” alisema Lissu.

Wadau wengine

Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa aliwataka viongozi wa Chadema kuendelea na kasi waliyoanza nayo ya kufanya siasa badala ya kufanya mikutano ya hadhara.

“Kwa spidi hii sijajua kama mnakaribia Dodoma au Magogoni. Mbowe anajua anachotaka na anajua anakokwenda,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba kuna vyama vingi vya siasa, lakini katika uchaguzi mkuu 2020, Chadema ndio tegemeo la Watanzania.

Samuel Malisa, alisema kupitia safu hiyo mpya anaamini Chadema inakwenda kuimarika kwa sababu viongozi waliochaguliwa wana mapenzi ya kweli na chama hicho.

“Mfano Katibu Mkuu Mnyika, naamini anakwenda kufanya vizuri katika nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake ndani ya chama. Pia wataweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu mwakani licha ya mazingira ya siasa kuwa magumu,” alisema.

Alisema Chadema imekuwa taasisi imara na kwamba imetoka gizani na sasa ipo imara kwa kazi ya kulikomboa taifa.

Ramadhani Khamis, alisema Chadema wamepata viongozi makini, wakweli, waaminifu, watiifu na wanaoona mbali katika kuliongoza taifa na kueleza kuwa yupo nyuma yao katika kuhakikisha wanafanikisha azma yao ya kuongoza nchi.