Chadema yakosa mawakala Serikali za mitaa, msimamizi asimamishwa

Thursday October 10 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar/Mikoani. Uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 jana umeendelea kwa kasi ndogo huku mambo kadhaa yakiibuka.

Moja ya mambo hayo ni pamoja na Chadema kutoweka mawakala katika vituo vingi mkoani Kilimanjaro kutokana na ukosefu wa fedha.

Sambamba na tukio hilo, msimamizi wa uandikishaji wapiga kura wilayani Uyui, Tabora alisimamishwa akidaiwa kuchanganya ujazaji fomu.

Msimamizi huyo, Columba Peter ambaye ni mkuu wa Shule ya Sekondari Kigwa ameondolewa kusimamia uandikishaji na kuvuliwa wadhifa wake na katibu tawala mkoa wa Tabora, Msalika Makungu.

Katika maelezo yake Makungu alisema Peter ameingiza taarifa tofauti na maelekezo yaliyopo katika daftari la uandikishaji na kusababisha waliojiandikisha kusaini sehemu yake na yao.

“Unakuta sehemu ambayo alipaswa asaini yeye wamesaini wapiga kura watarajiwa na huko kwao wameweka dole gumba, amechanganya na kuwapotosha watu wanaokuja kujiandikisha,” alisema Makungu na kumtaja, Fred Gama kusimamia uandikishaji.

Advertisement

Makungu alisema pamoja na kuondolewa katika nafasi hizo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tabora anatakiwa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kosa hilo.

Naye mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliagiza kuletwa kwa daftari jipya na kuandikisha upya watu wote waliokuwa wamejiandikisha na kuendelea na wengine kwa usahihi kulingana na maelekezo yaliyomo.

Mkoani Kilimanjaro vituo vingi vilikuwa na mawakala wa CCM pekee huku wakikosekana wa wapinzani wao wakuu Chadema.

Akizungumzia kutokuwepo kwa mawakala wa chama hicho, katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema alisema kwamba changamoto ni ukosefu wa fedha.

“Mfano manispaa ya Moshi vipo vituo 101 na kila kituo tunatakiwa kuweka wakala mmoja na siku saba si chache, tukisema kila wakala tumlipe Sh5,000 kwa siku ni fedha nyingi kwa siku zote.”

“Changamoto nyingine ni mfumo uliotumika kuweka mawakala, wametushtukiza, katika baadhi ya maeneo imetupa ugumu kuwapata mawakala, na kulazimika kuacha zoezi liendelee bila mawakala wetu,” alisema Lema.

Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Moshi, Lain Kamendu alisema katika manispaa hiyo kuna vituo 101 na waliapisha mawakala wa CCM na Chadema.

Wilayani Sengerema katibu mwenezi wa Chadema wilayani humo, Stanely Kakele aliwapongeza vijana kwa kujitokeza kwa wingi.

“Tukiendelea hivi hadi mwisho hakutakuwa na malalamiko yoyote na kutokana na namba ya vijana kuwa wengi kujiandikisha tuna imani tunashinda,” alisema Kakele.

Jijini Dar es Salaam kumekuwa na mwitikio mdogo na waandikishaji kuwaomba viongozi wa Serikali kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa kuwapatia elimu.

Shabani Ally mwandikishaji katika kituo cha Shule ya Msingi Yusuph Makamba iliyopo wilayani Temeke alisema tangu zoezi hilo lianze wamejiandikisha watu 300.

“Wapo wanaokuja kujiandikisha lakini si wakazi wa mtaa husika, huwezi kuwalaumu, tunachofanya ni kuwaelekeza katika kata zao ili wasikose haki ya kuchagua viongozi,” alisema Ally kauli iliyozungumzwa pia na mwandikishaji wa kituo cha Shule ya Msingi Mbagala, Lucas Robert.

Mkoani Morogoro wakuu wa wilaya, watendaji wa Serikali wametakiwa kusimamia uandikishaji huo ili ufanyike kwa amani na utulivu.

Mkuu wa mkoa huo, Loata Ole Sanare alieleza hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari akibainisha kuwa mkoa huo wanataraji kuandikisha watu milioni 1.4 sawa na asilimia 56 ya wakazi milioni 2.5.

Advertisement