Chui avamia kijiji, auawa

Wakazi wa Mugumu wilaya ya Serengeti wakiangalia Chui aliyeuawa baada ya kujeruhi watu saba, kula kondoo watano, mbuzi watatu na mbwa watatu katika kijiji cha Bisarara wilayani humo mkoani Mara. Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

  • Wiki moja iliyopita kabla ya chui huyo kuonekana na kula mifugo, wakazi wa kijiji hicho waliingiwa hofu ya wizi wa mifugo

Serengeti. Chui amevamia Kijiji cha Bisarara wilayani hapa na kujeruhi watu saba na kuua mifugo kumi wakiwimo kondoo watano, mbuzi watatu na mbwa wawili.

Tukio hilo lililotokea juzi ni muendelezo wa wanyamapori kuwa tishio kwa usalama na maisha ya binadamu na mifugo katika vijiji vya Wilaya ya Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).

Simba, fisi, chui na tembo ni miongoni mwa wanyamapori wanaovamia vijiji hivyo.

Uvamizi wa chui huyo aliyekuwa ameweka kambi kijijini hapo kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana alipouliwa na askari wanyamapori, umetokea kipindi ambacho wataalamu wa wanyamapori wanaendelea kuwasaka simba wanaodaiwa kuua mifugo 187 na kujeruhi watu kadhaa katika vijiji vya Makundusi na Parknyigoti.

Mkazi wa Kijiji cha Bisarara, Mairi Motera (40) ni kati ya watu wenye bahati baada ya kuponyoka mikononi mwa chui aliyemvamia wakati akiwa na jirani yake Mnyoro Gisoni wakifuatilia nyayo zake kwa sababu ya kuua mbwa wawili.

“Nikiwa nimeshika sime mkononi tayari kukabiliana na chui huyo, ghafla nilishtukia nimevamiwa na kupigwa kucha kwenye mkono wenye silaha; sikujua silaha ilivyoniponyoka. Nilipiga kelele za kuomba msaada na watu kujitokeza kuniokoa,” alisema Motera.

“Baada ya kuniokoa, watu waliendelea kumsaka chui ambaye alitokomea katikati ya shamba la mtama; ghafla tulisikia kilio cha Mwita Matiko (mwenzao) baada ya kuvamiwa na chui ambaye wakati huo alishakasirika na kutoa muungurumo uliotutia hofu.”

Alisema chui huyo aliyekuwa kajificha chakani, aliibuka na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, ndipo alipowajeruhi watu saba sehemu mbalimbali za mwili.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bisarara, Thomas Marwa alisema wiki moja iliyopita kabla ya chui huyo kuonekana na kuanza kujeruhi watu, wakazi wa kijiji hicho waliingiwa hofu ya wizi wa mifugo baada ya kondoo, mbuzi na mbwa kuripotiwa kupotea.

“Tulianza kuhisi na kufanya uchunguzi tukidhani kuna watu wanaiba mifugo; kumbe ni chui ndiye alikuwa anawakamata na kula kimya kimya,” alisema Marwa.

“Tunawashukuru askari wa wanyamapori na wale wa Gereza la Tabora B kwa kusaidia kumsaka na kumuua chui huyo dume,” aliongeza mwenyekiti huyo

Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu aliwataka wananchi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuchukua tahadhari muda wote wanapotembea maeneo yenye vichaka.

“Maofisa wanyamapori kutoka Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Tawa, Tawiri na Pori la Akiba la Grumeti wanaendelea na msako wa dhidi ya wanyamapori hao,” alisema Babu.