Daktari miaka 65 adaiwa kumuua mpenzi wake kwa wivu wa mpenzi

Thursday January 16 2020Kamanda wa Polisi Mara, Daniel Shillah

Kamanda wa Polisi Mara, Daniel Shillah 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kibondo. Matukio ya wapenzi kuuana au kujeruhiana yamezidi kujitokeza ambapo Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia Daktari wa Chama cha Msalaba Mwekundu (Red Cross), Albert Rugai (65) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake na yeye kufanya jaribio la kutaka kujiua.

Tukio kama hilo lilitokea Januari 9 mkoani Mara ambapo Juma Warioba (27) mkazi wa kijiji cha Butiama mkoani Mara alidaiwa kumuua mpenzi wake, Devotha Boniface (22) sababu ikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi baina ya wawili hao.

Kamanda wa Polisi Mara, Daniel Shillah alisema Warioba baada ya kudaiwa kutenda kosa hilo naye alikimbia ingawa alisakwa na kupatikana akiwa amejijeruhi kwa kisu tumboni na sasa yuko hospitalini kwa matibabu.

Alisema mtuhumiwa huyo alimchoma kwa kisu sehemu mbalimbali za mwili mpenzi wake na kusababisha kifo cha papo hapo akimtuhumu kuwa na uhusiano na wanaume wengine.

Wakati tukio hilo likiwa halijafutika, jana Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Otieno alizungumzia tukio la daktari wa Red Cross ambaye anadaiwa kumuua mpenzi wake kwa wivu wa mapenzi.

Alisema mauaji hayo yalitokea Jumapili iliyopita wilayani Kibondo ambako chanzo kinadaiwa ni wivu wa mapenzi baina yao.

Advertisement

Kamanda Otieno alisema kwamba mtuhumiwa alimpiga na nyundo kichwani mara mbili mpenzi wake aliyetajwa kwa jina la Esther Kondo (42) hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na ubongo kutoka nje.

Alisema hali hiyo ilisababisha Esther kupoteza fahamu na baadaye kufariki dunia akiwa ndani ya nyumba ya mpenzi wake huyo.

Kamanda Otieno alisema mtuhumiwa mara baada ya kuona hali hiyo imetokea alijaribu kunywa sumu na kujiua jaribio lililoshindikana na sasa yupo hospitali kwa ajili ya matibabu atakapopona atafikishwa mahakamani.

“Ninawashauri wananchi waache kujichukulia sheria mkononi kama unaona mpenzi wako ana shida achana naye na utafute mwingine usijitafutie matatizo kwani huyu mzee na umri wake anaenda kufia jela,” alisema Otieno.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibondo, Mathias Bwashi alikiri kupokea mwili wa marehemu huyo pamoja na mtuhumiwa anayedaiwa kufanya mauaji hayo.

Rugai sasa anapatiwa matibabu hospitalini hapo akiwa chini ya uangalizi wa polisi.

Advertisement