Dk Bashiru aibua joto la Tume Huru

Saturday January 11 2020

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Mwaka wa uchaguzi wa 2020 umeanza kwa mjadala mzito wa kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Madai ya Tume huru yanajirudia mara kwa mara kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo sasa inanyooshewa kidole na wadau, wakisema haiko huru.

Wanasema uongozi wake wote unateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni mwenyekiti wa chama kinachoshiriki uchaguzi – CCM.

Miongoni mwa wadau wanaopinga mfumo wa NEC wa usimamizi wa uchaguzi ni Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba, Bob Chacha Wangwe aliyeungua kesi akipinga Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia chaguzi na akashinda katika ngazi ya Mahakama Kuu, kabla ya kuanguka katika Mahakama ya Rufani kufuatia rufaa ya Serikali.

Mbali na Wangwe, suala hilo sasa limefikishwa mahakamani na Wakili wa kujitegemea Alex Masaba akipinga uteuzi wa Mkurugenzi mpya wa NEC, Dk Wilson Mahera na mmoja wa makamishna, Omar Ramadhan Mapuri.

Katika kesi hiyo namba 30 ya mwaka 2019, Masaba ambaye anajiwakilisha mwenyewe anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uteuzi wa viongozi hao wa NEC ni batili kwa kukiuka na kuvunja masharti ya katiba ya nchi na sheria ya NEC.

Advertisement

Viongozi hao wanadai kuwa au kuwahi kuwa makada wa CCM, na hivyo kukosa sifa za kuwa ndani ya NEC.

Madai hayo pia yamepewa kipaumbele na Chadema ambapo Katibu wake mkuu mpya, John Mnyika ametaja mahitaji ya Tume Huru kuwa katika mambo atakayoshughulikia.

Akizungumza Desemba 29, 2019 katika ofisi za Chadema Kanda ya Victoria, Mnyika alisema ili uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ufanyike kwa haki, wanataka yafanyike marekebisho ya mpito kwenye katiba iliyopo sasa kwa nia ya kuweka uwanja sawa wa uchaguzi.

Ili kufanikisha hilo anapendekeza iundwe Tume huru ya uchaguzi, kuwe na ibara inayotaka matokeo ya uchaguzi wa rais yapingwe mahakamani na kuwe na kifungu kinachosema ili mtu atangazwe kuwa mshindi wa urais awe amezidi asilimia 50 ya kura zote.

Madai ya Tume Huru ya uchaguzi ni miongoni mwa mambo yaliyopangwa kutiliwa mkazo na chama hicho katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Kutokana na kurudiwarudiwa kwa madai hayo ya Tume huru ya uchaguzi, kumemwibua Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akazungumzia suala hilo kwa kejeli kuwa “tume huru ya uchaguzi haipigi kura”, kauli ambayo imewaibua wadau wapya wakimsoa kupitia mitandao ya kijamii.

Kauli ya Dk Bashiru

Akizungumza hivi karibuni mkoani Kagera, Dk Bashiru amenukuliwa na ukurasa wa Twitter wa CCM akisema, “Wapo wanaolilia Tume Huru iwasaidie kupata ushindi. Tume huru haipigi kura bali inasimamia uchaguzi. Chama kisicho na wapigakura kisitegemee tume iwape ushindi. CCM imetafuta wapigakura kwa kutoa elimu bure, afya, maji na barabara, sasa wao waseme wapiga kura wamewapataje.”

Kauli hiyo imezua mjadala kwenye mtandao wa Twitter, ambapo baadhi ya wachangiaji wamehoji utekelezaji wa maendeleo unaofanywa na CCM na uhusiano wake na Tume ya Uchaguzi.

Mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Omar Said Shaaban anasema, “wapiga kura wetu ni wale victims (waathirika) wa matendo ya CCM na serikali yake. Waliokosa maji safi, afya bora, barabara nzuri, elimu nzuri, maisha magumu, waliokopwa mazao yao bila ya kulipwa, waliochoshwa na rushwa, na uonevu na ubaguzi.”

Armoured @EngNyahucho anasema: “Suala si ushindi, na kama mnaamini mnapendwa basi kubalieni tupate Tume Huru, woga wa nini na huku mna uhakika wa ushindi

Naye Clever Son Of Africa @AfricaClever anaandika: “Ni siasaaaa....au propaganda? Kwamba Bashiru hajui umuhimu wa Tume huru? Alipokuwa chuo kikuu kazungumza sana habari ya Tume Huru. Kwanini sasa hivi imegeuka? Kuwapo tume huru si hisani ya CCM, kwa nini wao walazimishe tume wanayoitaka wao. Tume huru ni lazima.

Msomaji mwingine, Think big @ThinkBigmind akasema, “So (kwa hiyo) kumbe hamfanyi hivyo kama ni sehemu ya kumfanya Mtanzania apate kile anachostahili ila mnafanya hivyo ili mpate wapiga kura. So (Kwa hiyo) leteni Tume huru halafu mtuachie Watanzania sisi wenyewe kisha ndiyo mtajua mlikuwa mnatafuta wapiga kura au mmevuruga wapiga kura mliokuwa nao.”

Si hayo, tu, Mickey’s Ismail @IsmailMickey akasema; “Katibu, kama tume huru haipigi kura kwa nini tusianzise mchakato wa kuwa na Tume Huru shida iko wapi? Tuingie kwenye uchaguzi huru ili wapiga kura wenu wawape ushindi.”

Mwingine anayejulikana kama PRINCE DEDITH @PrinceDideth anasema: “Wapo wanaolilia tusipate tume huru maana wamepoteza ushawishi kwa watu na chama. So (kwa hiyo) wanaogopa kukiwa na Tume Huru watanyolewa kwa chupa.”

Maoni kama hayo pia amekuwa nayo pia Joshua86 @JoshuaD28521800 akisema; “Wananchi (wapiga kura) ndio wanaotaka tume huru ya uchaguzi (tulitoa maoni yetu kwenye tume a Jaji Warioba (Joseph), mnatubaghaza kwa sababu mnadhani mko juu ya kila kitu. Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Eti wapinzani ndio wanadai tume huru! Wananchi tumewaambia.”

Naye leo @Meckyleo1 ameandika: “Kwa uelewa wangu pesa za kujenga nchi huwa zinatokana na kodi na siyo chama chochote. Hivyo mtu unapowekwa kuwa msimamizi wa jambo fulani usijimilikishe na kuanza kujigamba. Hii ni aibu kwa kweli. Ila shida ni wananchi kutojua haya mambo yanakwendaje, usimamizi mzuri huleta upendo.”

Advertisement