Dk Bashiru aonya kauli tata za makada CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally

Mwanza/Dar. Wakati wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wakikemea kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa zinazotishia maisha ya watu wanaodaiwa kuwa ni wasaliti wa Taifa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally naye ameonya juu ya kauli hizo tata.

Kauli hizo zimeshitua kiasi cha baadhi ya wadau kutaka vyombo vya dola na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kukemea na kuchukua hatua ili kudumisha umoja wa taifa na kuepusha mifarakano katika jamii kwa misingi ya siasa.

Haja ya kuepusha matamshi hayo yanayoweza kuzaa chuki ni muhimu ukizingatia mwaka huu unafanyika uchaguzi mkuu, ambapo nchi itachagua Rais, wabunge na madiwani.

Juzi, katika mitandao ya kijamii kuna video iliyokuwa ikizunguka ikimuonyesha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), mkoani Iringa, Kennani Kihongosi akisema kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anastahili kuuawa kwa usaliti.

Dk Bashiru akizungumza kwa simu na Mwananchi jana alisema, chama chake hakiwezi kuhimiza uovu nchini kama watu wanavyotafasiri kauli zinazotolewa mitandaoni na baadhi ya vijana wa chama hicho.

Alisema CCM ndiyo iliyoiweka Serikali madarakani na iko mstari wa mbele kuielekeza kuongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na Sheria na si kuvunja sheria.

“Hizi kauli zinazotolewa mitandaoni si ajenda ya chama chetu, CCM ina wasemaji wake wakuu na mnawafahamu, hawa viongozi wadogo wakizungumza huko na kuchukuliwa kuwa ndiyo kauli ya chama, mnakosea,” alisema Dk Bashiru.

Akitolea mfano wa video ya Kihongosi, Dk Bashiru alisema, “Kwanza haijawekwa yote mtandaoni, imekatwa kipande kidogo tu kinacholenga upotoshaji. Hivi mtu akimwambia mwanasiasa mwenzake ambaye wanapingana kuwa nitakuua kisiasa, ndiyo inamaanisha anataka kumtoa uhai? Hapana huyu anakuwa na maana ya kumuondoa kwenye ulingo wa kisiasa na ndicho alichokisema yule kijana kiongozi wa UVCCM Iringa kuwa ‘watamuua’ Zitto (Kabwe) kisiasa na si kumuondolea uhai kama ilivyotafasiriwa.”

Lakini pia kama chama, tunatambua kuna majibu ya mihemko miongoni mwa vijana wetu wanayoipata huko mitandaoni kutoka kwa vijana wenzao wa upinzani.

“Nikiona huwa nazungumza nao, wanifafanulie walikuwa wanamaanisha nini. Na tayari nimeshawaelekeza wawe makini kujibizana na kauli zinazotolewa mitandaoni na wapinzani na tayari wamenielewa na tutaendelea kuelimishana,” alisema Dk Bashiru.

Alisema vyombo vya habari navyo vitafakari kwa kina kauli zinazotembea mitandaoni kwa sababu nyingi zinalenga upotoshaji na kama zitabebwa hivyo hivyo, watawapotosha wananchi.

Dk Bashiru alisema hivi sasa nchi inakabiliwa na mambo mengi yanayotakiwa kuchukuliwa hatua ili kuwanusuru Watanzania wengine wanaopambana nayo.

Alitolea mfano wa mafuriko yanayoendelea kuwakumba wananchi katika maeneo mbalimbali, mvutano wa mkopo wa Benki ya Dunia na vifo vya watu 20 vilivyotokea Moshi kuwa yote haya yanatakiwa kujadiliwa kwa kina ili yapatiwe ufumbuzi.

“Lakini ajabu tunakimbizana na mambo yanayozushwa mitandaoni, tunapoteza muda. Hatuwezi kuwa na chama kikubwa kama CCM eti kikahimiza uvunjifu wa amani au kuhimiza mauaji, hili litakuwa jambo la ajabu sana. Vyombo vya habari mtusaidie kufafanua mambo haya,” alisema.

Chanzo cha kauli hizo

Februari 2, 2020, Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James alisema chama hicho kinawadekeza wapinzani alipokuwa akihutubia vijana jijini Arusha, “Wapinzani wa nchi hii tunawadekeza sana na mtoto ukimdekeza atakojoa kwenye kikombe cha kahawa na sisi vijana hatuwezi kukubali kuona watu hawa wakidekezwa.”

Kauli za viongozi hao zilitokana na kitendo cha Zitto kuiandikia barua Benki ya Dunia akiitaka izuie mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kugharamia elimu nchini.

Mkopo huo ulizusha mjadala mkali miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya wanaharakati wakihoji sababu ya Benki hiyo kutoa fedha kwa Serikali ilihali inapinga wanafunzi wa kike wanaopata mimba kuendelea na masomo.

Hata hivyo, Kihongoti alisema; “Watu wamenielewa vibaya, sikumaanisha Zitto auawe kwa kuondolewa uhai; bali nilimaanisha auawe kisiasa kuanzia kwenye nafasi yake ya ubunge na majukwaa mengine ya kisiasa yanayompa fursa ya kusema na kukiuka kwa umma.”