Dk Mashinji ahamia CCM

Muktasari:

Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vicent Mashinji leo Jumanne Februari 18, 2020 amehamia CCM na kupokewa na katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala nchini Tanzania, Humphrey Polepole.

Dar es Salaam. Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vicent Mashinji leo Jumanne Februari 18, 2020 amehamia CCM na kupokewa na katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala nchini Tanzania, Humphrey Polepole.

Dk Mashinji amejiunga CCM katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam ikiwa imepita miezi miwili tangu ufanyike mkutano  mkuu wa Chadema na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutompendekeza tena kuwa katibu mkuu.

Badala yake, Mbowe alimpendekeza mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa tano wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kupigiwa kura na baraza kuu.

Baada ya kukosa nafasi hiyo, Dk Mashinji alieleza masikitiko yake kwamba alitamani kuendelea kuwa katibu mkuu ili aweze kumalizia mipango aliyokuwa nayo, ikiwemo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.

Katika maelezo yake ya leo, Dk Mashinji amesema, “nimuombe mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kama ataridhia anipe nafasi ya kujiunga na CCM ili niweze kuchangia maendeleo ya nchi yangu.”

Amesema CCM ina nia ya kuwapa wananchi maendeleo tofauti na chama alichotoka, “ninaona kabisa CCM  kiko tayari kuwaendeleza Watanzania na kule nilikotoka huo utayari siuoni.”

Baada ya kueleza hayo, Polepole alimkaribish,“mimi nikuhakikishie kwa niaba ya wakuu wa chama wakiongozwa na ndugu Magufuli nimekupokea rasmi karibu sana CCM.”

 

 

Dk Mashinji ni nani?

Dk Mashinji alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Willibrod Slaa aliyeachana na chama hicho siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015.

Dk Mashinji ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu alichaguliwa baada ya jina lake kuwasilishwa na Mbowe  kwa Kamati Kuu ilipokaa chemba na baadaye mbele ya Baraza Kuu na kupitishwa kwa kura za kunyoosha mikono na kuwaacha wajumbe midomo wazi kwa kuwa awali walikuwa wanayazungumza majina mengine yaliyozoeleka.

Dk Mashinji alikuwa katibu mkuu wa nne wa Chadema tangu chama hicho kianzishwe baada ya Bob Makani, Dk Walid Aman Kabourou na Dk Slaa.

Dk Mashinji alizaliwa katika Wilaya ya Sengerema, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 mpaka Oktoba 1991 alipohitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kuanzia Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari. Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na mwaka 2007-2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).

Mwaka 2016 alikuwa mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii aliyosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria.