‘ETS itadhibiti udanganyifu wa mapato kipindi hiki cha vita dhidi ya corona’

Muktasari:

Serikali ya Tanzania ilitangaza mpango wake wa kuanza matumizi ya stempu za kielektroniki Juni 2018 na utekelezaji wa agizo hilo ulianza kufanyika Januari 15, 2019. Stempu hizo zilifungwa katika kampuni 19 zinazozalisha pombe, mvinyo na pombe kali.

Dar es Salaam. Kuanzishwa kwa matumizi ya stempu za kielektroniki (ETS) katika bidhaa tofauti Tanzania, kumeelezewa kuwa kutaisaidia Serikali ya nchi hiyo kukusanya kodi ya mapato ili kunusuru uchumi katika kipindi hiki ambacho Taifa limekumbwa na athari za corona.

Akizungumza na Mwananchi Jumatatu Machi 30, 2020, katika mahojiano kwa simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki alisema Serikali ilitangaza mpango wake wa kuanza matumizi ya ETS Juni 2018 ikiwa ni baada ya Kampuni ya Uswisi, Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA) kushinda tenda.

Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo hilo ulifanyika Januari 15, 2019, stempu hizo zilifungwa katika kampuni 19 zinazozalisha pombe, mvinyo na pombe kali.

Awamu ya pili ziliwekwa katika vinywaji baridi na chupa za maji kuanzia Agosti Mosi mwaka jana.

Ndaki alisema kupitia ETS hakuna kampuni inayoweza kuidanganya serikali kuwa haikufanya uzalishaji kutokana na athari ya virusi vya corona.

 “Katika kipindi hiki cha ugonjwa huu wa mlipuko wa virusi vya corona, ndiyo tunaona umuhimu wa ETS, ni muhimu kuliko kipindi chochote kwa sababu itaondoa mianya ya udanganyifu wa kodi,” alisema Ndaki.

Alisema kupitia stempu hizo, serikali pia ina uwezo wa kujua kiasi kinachozalishwa kwa kila bidhaa.

Awali, Kamati ya Bunge ya Bajeti ilifikiria mfumo huo unaweza kuwa kikwazo kwa serikali hasa linapokuja suala la ukusanyaji wa mapato.

 “Tulifikiri labda wazalishaji wanaweza kuuchezea mfumo huu na wakafanikiwa kukwepa kodi, lakini mfumo huu umetudhihirishia kuwa hilo haliwezekani na kodi inakusanywa bila tatizo,” alisema Ndaki.

Itakumbukwa, Desemba mwaka jana, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo alisema makusanyo yaliongezeka kutokana na kuanza kwa matumizi ya ETS.

Alisema Sh77.8 bilioni zilikusanywa kama ushuru wa bidhaa katika vinywaji baridi, pombe kali na mvinyo kati ya Februari na Oktoba mwaka jana.

Kiwango hicho kilikuwa sawa na ongezeko la asilimia 33.7 ikilinganishwa na Sh58.2 bilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2018.

Ushuru wa bidhaa wa vinywaji baridi uliongezeka kwa asilimia 8.7 hadi kufikia Sh10 bilioni kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2019 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2018.

 “Tunafanya kila linalowezeka  kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa sokoni zinakuwa na ETS,” alisema Mbibo na kuongeza;  “Timu yetu imejipanga kuhakikisha tunatekeleza yale tuliyokusudia.”

Pia, Mbipo alitumia nafasi hiyo kuiomba  Serikali kutoa motisha za kikodi na kiutawala ili kuongeza uzalishaji.

Alisema Serikali inatakiwa kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuweka kodi kubwa kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ilihali zinazalishwa nchini pia.

Alisema upendeleo maalumu unatakiwa kutolewa kwa wawekezaji wa ndani kusudi wapate hamasa ya kuongeza uwekezaji nchini.