Facebook na WhatsApp kubanwa kwenye iphone

Apple kuzibania apps za Facebook, WhatsApp na apps nyingine mbalimbali kwenye iPhone katika uamuzi unaoonyesha kuziathiri apps nyingine nyingi.

Apple wamesema wanafanya mabadiliko katika teknolojia ya simu zinazotumia internet (voice over internet protocol – VoIP). Katika mabadiliko hayo programu endeshaji ya iOS haitaruhusu apps zisizotumika kuendelea kufanya kazi nyuma ya pazia (background) kwenye iPhone. Apps kama vile Facebook, WhatsApp, Skype na zingine zinazotegemea teknolojia ya VoIP, kupiga simu kwa njia ya intaneti, zitaathirika na uamuzi huo.

Apps zinazotumia teknolojia ya simu kwa njia ya intaneti kama vile Facebook na WhatsApp huwa zinahitaji apps hizo ziendelee kufanya kazi hata kama mtumiaji wa simu hazitumii kwa wakati huo. Uamuzi huu wa Apple inasemekana umejikita zaidi katika suala la kulinda faragha ya watumiaji wa simu zake. Inasemekana bado apps hizo zikiwa zinafanya kazi nyuma ya pazia zimekuwa zikikusanya data kuhusu utumiaji wa simu wa mtu husika. Mabadiliko hayo yataanza kufanya kazi kwenye toleo la iOS 13 linalotegemewa kutambulishwa rasmi Septemba, 2019.

Watengenezaji apps hizo wamepewa hadi Aprili 2020 kuhakikisha apps zao zinafuata utaratibu huu mpya.