Finland yashughulikia changamoto ya utawala bora kwa staili tofauti

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akizungumza jambo na Waziri wa Ushirikiano wa Biashara wa Finland, Ville Skinnari baada ya kumaliza mazungumzo alipomtembelea ofisini kwake, jijini Dodoma juzi.  Picha na Wizara ya Fedha

Dar es Salaam. Finland imesema inaelewa changamoto za masuala ya utawala bora na demokrasia yanayoikabili Tanzania na kwamba inafuatilia, lakini inashughulikia suala hilo kwa njia tofauti na mataifa mengine.

Akizungumza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vya kampuni ya Mwananchi Communications yaliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Biashara ya Nje, Ville Skinnari alieleza kwa undani namna ambavyo nchi yake pia imo katika utekelezaji a mipango ya kuweka mkazo katika kufanya biashara na Tanzania badala ya kutoa misaada.

Mwananchi Communications ndio inayochapisha gazeti hili la Mwananchi na mengine mawili ya The Citizen na Mwanaspoti.

Skinnari aliwasili nchini Jumapili iliyopita na alikutana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango jijini Dodoma juzi.

Ziara yake ya Tanzania ni sehemu ya mpango wake wa kutembelea bara la Afrika, akiendelea na safari yake nchini Msumbiji.

Tanzania na Msumbiji zinatajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopokea misaada ya Finland kwa wingi.

Katika kipindi cha kuanzia 2019, Finland imetoa msaada katika kusaidia maeneo ya uendelezaji misitu na rasilimali, utawala bora, uvumbuzi na upangaji wa mipango ya maendeleo.

Utawala bora na demokrasia

Katika mahojiano ya juzi ambayo yalishuhudiwa pia na balozi Riita Swan, Skinnari alisema nchi yake imekuwa inafuatilia hali iliyo nchini Tanzania.

Matatizo inayoyaona ya masuala ya utawala bora yameainishwa pia katika tovuti ya ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

Matatizo hayo ambayo yameelezewa kuwa yanaipa ugumu Finland katika utekelezaji wa kimkakati wa shughuli zake nchini Tanzania ni pamoja na masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.

“Tunazifahamu changamoto na kilichoandikwa kwenye tovuti ya ubalozi wetu ni sahihi,” alisema waziri huyo katika mahojiano yaliyofanyika hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam.

“Hiyo ni baada ya utafiti uliofanywa na maofisa wa ubalozi wetu hapa nchini Tanzania na wale wa Wizara wa Mambo ya Nje wa Finland.

“Ninafahamu utendaji wao mzuri wa kazi. Ila jambo la muhimu kwetu ni kile tunachopata na tunachokifahamu huwa tunawasiliana na wenzetu wa Serikali ya Tanzania.”

Kushughulikia matatizo ya utawala bora

Kuhusu changamoto za utawala bora, Skinnari alisema tofauti na mataifa mengine, nchi yake hushughulikia matatizo ya Tanzania kwa njia tofauti.

Alisema wao wanaamini katika mazungumzo na kutoa mafunzo ili Tanzania iweze kuyakabiliana matatizo hayo.

Baadhi ya nchi tajiri duniani husitisha misaada kulazimisha kuondolewa kwa kasoro katika utekelezaji wa utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu.

Utawala bora ni eneo linalokamata nafasi ya pili katika mgao wa fedha za misaada na serikali ya Finland.

Wakati Tanzania ilipopokea Euro 52 milioni (Sh129 bilioni) kati ya mwaka 2016 hadi 2019, asilimia 39 ilikwenda katika masuala ya utawala bora.

Skinnari alisema kumekuwa na maendeleo katika eneo la utawala bora, ingawa alisema changamoto bado zipo.

“Hatua ya kwanza tunachofanya ni kuzungumza na wenzetu wa Tanzania kuwaambia kile tunachofahamu ili kusaidia kutatua matatizo hayo,” alieleza Skinnari.

Skinnari alieleza kuwa Finland ina namna yake ya kukabili matatizo ya Tanzania hayo ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu.

Alisema nchi yake haina mpango wa kufuata mtindo wa nchi nyingine wa kuibana Tanzania.

Mwaka juzi, Serikali ya Denmark ilitangaza kukata msaada wa dola 10 milioni (Sh 22.8 bilioni) kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa haki za binadamu nchini Tanzania.

Hivi karibuni Sweden ilitangaza kukata robo ya msaada wake wa dola 41 milioni (Sh94 bilioni) kwa Tanzania mwaka jana.

Ilieleza sababu ya kuchukua hatua hiyo ni kutoridhishwa na maeneo matatu ya usimamizi wa fedha za umma, rushwa na ufinyu wa demokrasia.

Marekani nayo hivi karibuni ilitangaza kumzuia mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuingia nchini humo, ikimhusisha na kukiuka haki za binadamu hiyo ni baada ya kusisitiza haja ya Tanzania kuwa na uchaguzi huru.

Utoaji wa mafunzo

Skinnari alisema njia nyingine wanayoitumia kuisaidia Tanzania kuinua kiwango chake cha masuala ya utawala bora ni kutoa mafunzo.

Aliyataja maeneo waliyojikita katika kusaidia mafunzo ni pamoja na usimamizi wa fedha za umma, kuboresha mfumo wa kodi, mafunzo kwa viongozi wa umma, kujenga uwezo wa wanawake kushiriki katika vyombo vya uamuzi na uwezo wa watu wa kupata habari na ushiriki wao katika kupata haki zao.

“Pamoja na jitihada hizo, ukweli unabakia kuwa bado kuna changamoto nyingi,” alisema Skinnari.

Twaweza waula

Waziri huyo pia alizungumzia msaada wa Finland kwa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza.

Serikali ya Finland ni miongoni mwa wafadhili wa taasisi na mkataba wao wa kufadhili Euro 350,000 (Sh799 milioni) ulikuwa unamalizika mwishoni mwa mwaka huu na kwamba wana mpango wa kuongeza ufadhili huo.